Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maslahi ya chama yawaengua wagombea urais NCCR-Mageuzi, wajumbe waduwaa
Habari za Siasa

Maslahi ya chama yawaengua wagombea urais NCCR-Mageuzi, wajumbe waduwaa

Abubakari Juma
Spread the love

WANACHAMA watatu wa chama cha NCCR-Mageuzi, wamejitoa kuwania urais urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 28 Oktoba 2020 kwa kile walichoeleza kuweka mbele maslahi ya chama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Waliojitoa ni Abubakari Juma, Peterson Mushenyera na Samuel Ruhuza na aliyebaki kwenye nafasi hiyo ni Yeremia Kurwa Maganja.

Pia, Haji Hamisi naye amejitoa kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar hivyo kutokuwa na mgombea yeyote katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika 27 na 28 Oktoba 2020.

Hayo yametangazwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Anthony Komu mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika leo Ijumaa tarehe 7 Agosti 2020 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, katika maelezo yao, hawakuweka wazi hasa, maslahi ya chama wanayozungumza ni yapi huku wajumbe waliozungumza na MwanaHALISI Online ukumbini hapo wakishindwa kuelewa hasa sababu zilizowafanya wajitoe ni zipi.

 

“Hatujajua kwa nini wamejitoa, inakuwaje wanajitoa siku ya mwisho kabisa tena ukumbini. Ukiwasikiliza sababu zao kama sizielewi elewi hivi,” amesema mjumbe mmoja wa mkutano huo kutoka Dar es Salaam

Mjumbe mwingine kutoka Kigoma amesema “sisi tulijua Ruhuza atashinda, sasa sijui kwa nini amejitoa, kikubwa kuna kitu ambacho hatujakijua labda tutaambiwa baadaye ila kwa sababu walizotoa hatujazielewa kabisa.”

Baada ya taarifa hiyo ya Komu na kueleza mgombea Abubakari hakufika ukumbini hapo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliwaita watiania waliokuwepo kila mmoja kuzungumza mbele ya wajumbe hao.

Hamisi amesema, ameamua kukaa kando kutokana na umri wake na siasa za Zanzibar zilivyo inamuwia vigumu hivyo kuwaomba wajumbe wa mkutano huo kumwelewa.

Naye Mushenyera amesema, “nilitia nia kugombea urais wa Tanzania. Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, sifa zote ninazo lakini kwa kuzingatia maelewano na amani. Nilipokuja kuchukua fomu, nilijua nitakuwa mwenyewe.”

“Lakini uchaguzi ni mchakato, lakini tulipokwenda katika kikao na kushauriana, kukawa na wengine na mimi chama hiki nakipenda sana, niliingia katika chama hiki Julai 1992 na watu wengine tulioanza, walikwenda chama hiki na kurudi lakini mimi sijawahi kuhama,” amesema.

“Nashwishika kusema, chama hiki kiendelee kukuwa na kuwa na amani, kwa hiyo, baada ya kutafakari, kushauriana na wenzangu, kutoka katika safu ya moyo wangu, nikaona nimuunge mkono Yeremia Maganja na ninaomba wapambe wangu munielewi vizuri, uchaguzi umepasua vyama, unaleta makundi, sisi katika NCCR-Mageuzi tumelelewa, hatuwezi kupasua chama chetu,” amesema Mushenyera.

 

Amewaomba, wale waliokuwa wanamuunga mkono kuhamishiwa ushirikiano wao kwa Maganja.

Mushenyera amemwomba, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Sisty Nyahonza ambaye ni miongoni mwa wahudhuriaji wa mkutano huo kwenda kuwaeleza watawala wajiandae kukabidhi madaraka.

“Mwaka 2020 katika historia ya Tanzania, msajili nenda kawaambie watawala kwamba mgombea wa NCCR-Mageuzi atashinda, tunaomba uwashauri sasa wanaotawala sasa wakabidhi kwa NCCR-Mageuzi.”

“Najua watawala wa sasa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa sasa ni John Pombe Magufuli. Mimi nilikuwa na mbinu lakini siri hizo hizo nazihamishia kwa Maganja, tutamshinda kwa kishindo, tutamshinda kwa kishindo,” amesema

Kwa upande wake, Ruhuza akizungumza taratibu amesema “nimekuwa katika chama hiki tangu kimeanza mpaka sasa, wengine wameondoka, sisi tupo. Nilijaza fomu za kuomba kugombea urais wa Tanzania kwa sababu niliona natosha na sifa zote ninazo na nilichokifanya katika chama changu kila mtu anakiona.”

 

Ruhuza aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho amesema “kwa nguvu na ushawishi nilioanao, ndiyo ulinifanya nijaze fomu. Kitu kimoja huwa nalinda zaidi maslahi ya chama, hiki chama tumekianza mbali, tumepita katika mazingira yote ni lazima tufike mbele na nitashukuru kikifika na mimi nikiwepo.”

“Ili wote tuje pamoja, tuje sambamba, ulikuwa mjadala mrefu, lakini kama nilivyosema, kwa maslahi ya chama, kuna watu walianza kunipongeza mapema hata kabla ya uchaguzi huu, lakini nilikuwa najiuliza nikitoka hapa (baada ya mashauriano) nitawaambia nini, lakini nimeona niweke mbele maslahi ya chama.”

Ruhuza amesema “wote tuna lengo moja, wote tunahitaji ushindi, NCCR-Mageuzi iwe mbele kuliko mtu, kwa hiyo, kwa maslahi mapana ya chama, bila kumung’unya maneno niseme kwamba narudi nyuma ili mmoja asonge mbele ili kuleta ushindi wa chama chetu.”

Akihitimisha maelezo yake, amesema “ili tukienda kuongoza, tuwe pamoja. Najua wengi mtasononeka lakini nimeona niweke mbele chama ili kupata ushindi wa chama, chama kiweze kuongea zaidi kuliko maslahi ya kwetu.”

Akijinadi mbele ya wajumbe hao, Maganja amesema “Nimependeza kuona hekima ya wagombea wenzangu wameamua kuniunga mkono, niko mbele yenu kuwaomba kura ili tushirikiane kwa pamoja kupeleka sera yetu iliyoshiba kwa wananchi ili waweze kutuchagua kwa ngazi zote tatu za udiwani, ubunge na urais.”

“Ninao uzoefu wa kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali kupitia siasa na utafiti na shughuli mbalimbali. Ninajua mkulima anataka nini, wafanyakazi wanahitaji nini na kwa kushirikiana nanyi kwa uzoefu niliona nao, tukiwa pamoja tutashinda,” amesema Maganja

Sasa shughuli ya uhesabuji wa kura zinaendelea.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu ya kijamii kwa taarifa na habari mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!