October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mapambano dhidi ya Corona: Madaktari waiangukia serikali, wananchi

Dk. Elisha Osati, Rais wa MAT

Spread the love

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeiomba serikali na wananchi kutoa ushirikiano kwa watalaamu wa afya, katika mapambano dhidi ya mlipuko wa Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu, inayosababishwa na Viysi vya Corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa jana tarehe 2 Aprili 2020 na Dk. Elisha Osati, Rais wa MAT, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Tunaomba serikali na wadau wote nchini kuelewa na kutambua mchango wa watumishi wa sekta yetu. Serikali ihakikishe uwepo wa vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi kama barakoa (Mask N95), ni muhimu sana kwetu ukizingata idadi ya wagonjwa na walio katika hatari ya kupata maambukizi ya COVID-19, ikiwa inaongezeka siku hadi siku. Hivyo tahadhari ni muhimu,” amesema Dk. Osati.

“Pia tunapendekeza kupunguzwa wagonjwa kwenye kliniki zetu mbalimbali kwa kutoa dawa za muda mrefu, walau miezi mitatu, ili kupunguza mlundikano wa wagonjwa kwenye kliniki zetu. Kwa sababu hawa wana uwezekano wa kupata ugonjwa mkali zaidi wa COVID-19,” ameshauri Dk. Osati.

Dk. Osati amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa afya ,kwa kufuata maelekezo yanayotolewa juu ya udhibiti wa ueneaji wa ugonjwa huo.

Akijibu maombi hayo, Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, amesema serikali imepokea ushauri wa MAT  na kwamba itaufanyia kazi.

“Ushauri umepokelewa, Na kuhusu kupunguza idadi ya wagonjwa wa kliniki katika hospitali zetu, kama nilivyoahidi jana, tutalifanyia kazi na tutatoa mrejesho haraka,” ameahidi Waziri Ummy kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali, Tanzania ilikuwa na wagonjwa 20 wa COVID-19, mmoja kati yao amefariki dunia huku mmoja akipona, na kubaki na wagonjwa 18.

Pia, serikali inafuatilia watu 532 wanaoshukiwa kukutana na waathirika wa ugonjwa huo, wakati watu 136 wakiwekwa Karantini, huku watu 176 wakimaliza siku 14 za kukaa karantini.

error: Content is protected !!