HATIMAYE Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Hayati Edward Lowassa, umewasili nyumbani kwake Ngarash wilayani Monduli mkoani Arusha kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa fursa kwa wakazi wa mji huo kutoa heshima za mwisho na kukamilisha taratibu za maziko. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Msafara wa mwili huo uliowasili nyumbani hapa saa 8:50 mchana, ulipokewa kimyakimya bila vilio kutoka kwa mamia ya wakazi wa kijiji cha Ngarash, mkoa wa Arusha, viongozi na wageni mbalimbali.
Licha ya baadhi ya wananchi kutamani kugusa jeneza la mwili huo, hawakufua dafu kwani walinzi walihakikisha mwili huo umepelekwa katika nyumba maalumu iliyoandaliwa nyumbani kwake kwa maandalizi mengine.
Lowassa aliyefariki dunia tarehe 10 Februari mwaka huu, akipatiwa matibabu kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) , baada ya kuugua kwa muda mrefu, mwili wake unatarajiwa kuzikwa Jumamosi ijayo tarehe 17 Februari mwaka huu.
Mamia ya wakazi wa Arusha na Monduli walisimama pembeni ya barabara ambazo mwili wa Lowassa unapitishwa, kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho.
Mwili wa Lowassa unatarajiwa kuagwa na wananchi kesho Ijumaa, kisha kuzikwa Jumamosi ambapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kushiriki mazishi hayo.
Enzi za uhai wake, Hayati Lowassa alifanikiwa kukonga nyoyo za watanzania wengi alipokuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata alipohamia chama cha upinzani cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Leave a comment