WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemuagiza Naibu wake, Dotto Biteko, kutafuta muarobaini wa changamoto ya uhaba wa mafuta ndani ya siku saba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo bungeni jijini Dodoma, akimjibu Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, aliyehoji hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini wakati wote na kwa gharama nafuu.
Katika agizo lake hilo, Waziri Majaliwa alimtaka Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, kufanya kikao na taasisi zinazoshughulika na biashara ya mafuta, pamoja na wafanyabiashara, kuona namna ya kupanua wigo wa uagizaji wake, ili nchi iwe na akiba ya kutosha.
“Ili watanzania wapate huduma hiyo muhimu ya upatikanaji wa mafuta, wanunuaji na taasisi ya uuzaji wa mafuta mtengeneze kikao kikubwa na wizara zinazohusika. Mkae muone namna ya upatikanaji wa mafuta.

“Tupanue wigo wa waagizaji mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa taifa letu na kama hii itafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumepata majibu na tutawapa taarifa watanzania na naibu waziri mkuu atashughulikia hilo,” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Majaliwa amesema Biteko ameshaanza kufanya vikao kadhaa na wadau kwa ajili ya kutafuta suluhu ya changamoto hiyo, iliyokuwepo tangu January Makamba, alivyokuwa Waziri wa Nishati.
“Kufuatia mabadiliko ya Rais Samia Suluhu Hassa aliyoyafanya juzi, tumeanza kumuona naibu waziri mkuu akifanya vikao kadhaa na wizara na kukutana na wadau. Kwa kuwa ameshaanza hii kazi niendelee kumuagiza kushughulikia suala hili zaidi mafuta yapatikane nchini, suala la bei tunajua zinabadilika wakati wote,” amesema Waziri Majaliwa.
Leave a comment