October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama ya Afrika: Matokeo urais Tanzania yapingwe mahakamani

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kufanyia marekebisho Ibara ya 41 (7) ya Katiba yake, inayopinga matokeo ya rais kupingwa mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Amri hiyo imetolewa leo Jumatano tarehe 15 Julai 2020 na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR), kupitia hukumu yake juu ya Kesi Na. 18/2018, iliyofunguliwa na Wakili Jebra Kambole dhidi ya Serikali ya Tanzania.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2018 mahakamani hapo, ilipinga kifungu hicho cha Katiba, kwa madai kwamba kinakiuka Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu, Ibara ya 1, 2 na 7 (1).

Katika utetezi wake, Wakili Jebra alidai, Ibara ya 41 (7) inakiuka haki ya usawa mbele ya sheria, haki ya kutobaguliwa pamoja na haki ya kusikilizwa  katika vyombo vya maamuzi, kinyume na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu, ambao Tanzania iliuridhia.

Ibara hiyo 41 (7) inasomeka, “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Baada ya utetezi huo, AfCHPR imeiamuru Serikali ya Tanzania kufanyia marekebisho ibara hiyo, kisha ipeleke kwenye mahakama hiyo ripoti ya utekelezwaji wa amri hiyo, ndani ya muda wa miezi 12.

Pia, AfCHPR imeamuru Serikali ya Tanzania kuchapisha hukumu hiyo katika tovuti yake rasmi, pamoja na ya mahakama kisha ikae ndani ya muda wa mwaka mmoja, ili wananchi waisome.

error: Content is protected !!