Wednesday , 8 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli atoboa siri yake na Balozi Kijazi
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli atoboa siri yake na Balozi Kijazi

Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Magufuli
Spread the love

 

SAFARI ya ushirikiano baina ya Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wake, Balozi John Kijazi, ilianza tangu mwaka 1995. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Ijumaa tarehe 19 Februari 2021, na Rais Magufuli wakati anaelezea historia ya marehemu Balozi Kijazi (64), katika ibada ya kuuaga mwili wake, iliyofanyika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Balozi Kijazi alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021 saa 3:10 usiku, wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma, na mwili wake unatarajiwa kuzikwa Jumamosi ya terehe 21 Februari 2021, nyumbani kwao Korogwe mkoani Tanga.

Akielezea namna alivyomfahamu marehemu Balozi Kijazi ambaye aliwahi kuwa Mhandisi wa Barabara mkoani Dodoma, Rais Magufuli amesema, kwa mara ya kwanza alikutana nae mwaka 1995, wakati yeye alipokuwa naibu waziri wa ujenzi.

https://www.youtube.com/watch?v=pNTE58LJ7bg

Rais Magufuli wakati huo aliteuliwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, kuwa naibu waziri wa ujenzi.

“Balozi Kijazi nina historia naye ndefu kidogo, wakati nimechaguliwa na Mzee Mkapa kuwa naibu waziri wa ujenzi 1995, nilitembelea maeneo mengi ya barabara na nikakutana na wahandisi wengi waliokuwa wa mikoa wakati huo na wengine wako hapa.”

“Nilipotembelea barabara za Dodoma nikakuta zote zinapitika pamoja zilikuwa na vumbi, nikaamuliza Balozi Kijazi, kwa nini zako nzuri kuliko za wahandisi wengine wa mikoa wakati fedha zinatolewa zilezile,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, katika ziara yake mkoani Dodoma, aligundua utendaji mzuri wa Balozi Kijazi, uliomshawishi kumpigia debe kwa aliyekuwa waziri wa ujenzi, Anna Abdallah, amteue kuwa mhandisi mwandamizi wa ujenzi wa barabarani ndani ya wizara hiyo.

“Niliporudi wizarani, nikatoa ushauri wangu kwa waziri wangu wakati huo, Mama Anna Abdallah, kwamba nimegundua kuna mhandisi mmoja anafanya kazi nzuri sana na barabara zake nzuri.”

Rais Magufuli amesema “kama ameweza kufanya mkoa mmoja wa Dodoma, naomba tum-promote awe mkurugunzi afanye matengenezo ya barabara zote Tanzania.”

Rais Magufuli amesimulia “Mama Anna akanikubalia na ndipo Balozi Kijazi akateuliwa kuja Dar es Salaam, akawa anashughulikia bararaba zote za Tanzania, na nyingi zilikuwa zinapitika na yeye alikuwa hakai ofisini anatembelea barabara zake.”

Imani ya Rais Magufuli kwa Hayati Balozi Kijazi haikuishia hapo, mwaka 2000 baada ya kuteuliwa na Hayati Mkapa kuwa waziri wa ujenzi na uchukuzi alimpendekeza Balozi Kijazi kuwa katibu mkuu wa wizara huyo.

Rais Magufuli amesema, alijitoa mhanga kwenda Ikulu jijini Dar es Salaam, kumuomba Hayati Mkapa amteua Balozi Kijazi, kuwa katibu mkuu wizara ya ujenzi.

“Nikamuomba Mzee Mkapa, huyu ambaye ni mkurugenzi wa barabara awe katibu mkuu wizara ya ujenzi, nilifanya hivyo nikijua nafanya makosa, na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete anafahamu hili. Lakini niliona nijilipue nimueleze tu Mzee Mkapa, aliniangalia nafikiri alinishangaa, hakunipa jibu,” ameseama Rais Magufuli.

Rais John Magufuli

Rais Magufuli amesema “mwaka 2002, Balozi Kijazi akawa ameteuliwa kuwa katibu mkuu, amefanya kazi kweli. Kazi nyingi zimefanyika, barabara nyingi zilitengenezwa kipindi chake.”

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, miaka mitano baadaye, baada ya kuondoka wizara ya ujenzi na kuhamishiwa wizara ya ardhi, mwaka 2007 Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alimteua marehemu Balozi Kijazi kuwa Balozi wa Tanzania katika Nchi za India, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal.

Ambapo makazi yake yalikuwa New Delhi India

“Alipoingia India, amefanya mengi na akaifanya India kuwa karibu sana na Tanzania, na mpaka waziri mkuu wa India akaja akatembelea Tanzania, nafikiri Mzee Kikwete akatembelea India na nchi nyingine, sababu ya kazi nzuri sana aliyoifanya Balozi Kijazi,” amesema Rais Magufuli.

Marehemu Balozi Kijazi alihudumu katika ubalozi huo kwa miaka tisa kuanzia 2007 hadi 2016, alipoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

“Nilipochaguliwa kuwa rais, nimetafuta nani atanisaidia kuwa katibu mkuu kiongozi, nikaamua kumuita kutoka ubalozini akawa katibu mkuu kiongozi. Najua watendaji wenzangu, watakubaliana name, sikufanya makosa” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, kifo cha Balozi Kijazi, kimeacha pigo kwa Serikali ya Tanzania, kwa kuwa alikuwa kiongozi mahiri, mnyeyekevu na mwenye upendo.

“Kwangu mimi na watendaji wote ndani ya serikali tumepoteza mtu muhimu sana, alizaliwa 1956 mpaka leo alikuwa katibu mkuu kiongozi, maana yake wakati wa kustaafu mwaka 2017 nikajaribu kutafuta replacement (kubadilisha) nikakosa nikamwongeza miaka miwili.”

“Nikafikiri baada ya miaka miwili nitapata mwingine, ikafika 2019 sikupata nikamuongeza tena miwili, Mungu amesema umezoea sasa ngoja akamtumie mwenyewe,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, kuna baadhi ya viongozi aliowateua, wameendelea kuwa kwenye nafasi zao kutokana na ushauri aliokuwa akipewa na Balozi Kijazi pindi alipotaka kuwatumbua akimnukuu akimwambia pindi alipotaka kuwatumbua “Mheshimiwa Rais, mpe siku mbili anaweza kubadilika” hivyo, kuondoka kwake ni pigo kubwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!