May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mpango mgonjwa, Magufuli asoma ‘sms’ aliyotumiwa

Spread the love

 

JOHN Magufuli, Rais wa Tanzania, amelazimika kusoma hadharani ujumbe aliotumiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, ili kukanusha taarifa za uongo zilizodai waziri huyo amefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Magufuli amesoma ujumbe huo leo Ijumaa tarehe 19 Februari 2021, kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, katika Ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, aliyefariki dunia tarehe 17 Februari mwaka huu, Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, zilisambaa taarifa za uongo zilizodai Dk. Mpango amefariki dunia.

Kufuatia uvumi huo, Mkuu huyo wa nchi amesema, Dk. Mpango ni kweli amelazwa hospitalini jijini Dodoma na leo asubuhi, alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi, akimjulisha kwamba anaendelea vizuri na matibabu.

“Tumefikia mahali tunatishana sana, leo nilitumwia meseji na Waziri wa Fedha, Dk. Mpango ambaye amelazwa Dodoma, na ninaomba niisome hapa kwa faida ya wale waliokwua wana-Twitte kwamba amekufa,” amesema Rais Magufuli.

Baada ya kauli hiyo, alitoa simu yake mfukoni na kuanza kuusoma “Leo asubuhi ananiambia mheshimiwa rais, ahsante sana, nimepata ujumbe wako kupitia mke wangu, kwa neema ya Mungu naendelea vizuri. Ninakula, nafanya mazoezi ya kifua na kutembea.”

Kuhusu watu waliomzushia kifo Dk. Mpango, Rais Magufuli amesema waziri huyo amewaombea msamaha kwa Mungu.

Rais Magufuli amenukuu ujumbe huo wa Dk. Mpango uliosema “hao wanaonizushia kifo kwenye mitandao, niliwaombea msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.”

“Huyo ambaye aliambiwa jana amekufa, yeye amesema katika sala yake jana jioni aliwaombea msamaha kwa Yesu,” amesema Rais Magufuli

error: Content is protected !!