Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Madudu ya uchaguzi 2019, 2020 yawatesa wapinzani
Habari za Siasa

Madudu ya uchaguzi 2019, 2020 yawatesa wapinzani

Wapiga kura
Spread the love

MADUDU yaliyojitokeza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020, bado yanaendelea kuwatesa wanasiasa wa vyama vya upinzani, licha ya Serikali kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi ili kuboresha mifumo ya uchaguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Miongoni mwa dosari zilizolalamikiwa na wapinzani ambazo zilijitokeza katika chaguzi hizo ni, kura za kughushi kudaiwa kutumbukizwa katika sanduku la kupigia kura, baadhi ya mawakala wa wagombea wa upinzani kuzuiwa kuingia kwenye vyumba vya kupiga kura, wagombea kukatwa bila sababu za msingi na madai ya wasioshinda kutangazwa washindi.

Akizungumza katika mdahalo wa kujadili chaguzi zijazo, leo Jumatatu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim Lipumba, amesema hawajui kama marekebisho ya sheria hizo yataweza kudhibiti dosari hizo ili zisijitokeze tena.

“Ukitazama uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019 ulivyokua mpaka sasa hatujui kanuni za uchaguzi wa mwaka huu zitakuwaje, kwa hiyo unaanza kupata wasiwasi kidogo kwamba je, uchaguzi wa 2024 utakuwa kama wa 2019? Ama utakuwa tofauti?” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema “Uchaguzi Mkuu wa 2020 ulivyokuwa na tulivyoshiriki mazingira yaliyokuwepo na kwamba Tanzania bara vyama vya upinzani viliweza kupata viti viwili kati ya 214, lakini pana mabadiliko ya sheria yamepitishwa lakini hatuna uhakika utekelezaji wake ukoje na kwamba mazingira gani tutakuwa nayo katika uchaguzi wa 2025.”

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Taifa, ameonesha wasiwasi huo baada ya mjadala huo kujikita juu ya namna ya kushawishi vijana kushiriki chaguzi zijazo hasa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Prof. Lipumba amesema mjadala huo utapaswa kuangalia namna ya kuhakikisha marekebisho ya sheria za uchaguzi yaliyofanyika yanaondoa changamoto zilizojitokeza kwenye chaguzi zilizopita.

“Lakini mazungumzo haya yananipa moyo sababu sote tunashiriki, yanaweza leta mawazo juu ya namna gani katika uhalisia tulio nao tunaweza kusukuma mabadiliko ambayo yamepitishwa kuwa chanya. Tukaweza kuwa na siasa na demokrasia na kwamba wapiga kura wakashiriki kupiga kura na kura hizo zitahesabiwa na matokeo kila mmoja anaamini haya ni matokeo halali na yanaonesha matakwa ya wapiga kura,” amesema Prof. Lipumba.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa upinzani kuonesha wasiwasi wao juu ya chaguzi zijazo kama zitakuwa huru na za haki, kwani kuna baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo CUF na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), viligoma kushiriki chaguzi za ndogo hadi madai yao juu ya uobreshaji mifumo ya uchaguzi yatakapofanyiwa kazi.

1 Comment

  • Ni mpaka chui atakapoweza kuamua kwa haki kesi kati ya mwana-mbuzi na mtoto wa chui. Sasa sijui itakuwa lini hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!