Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lowassa: Mwanasiasa aliyetikisa CCM, Chadema
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Lowassa: Mwanasiasa aliyetikisa CCM, Chadema

Spread the love

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa (70) amefariki Dunia tarehe 10 Februari 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini (JKCI) Dar es Salaam.

Akitangaza kifo hicho kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia televisheni ya Taifa (TBC), Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesema Lowassa amefariki saa nane mchana.

Lowassa alikuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la  damu.

“Lowassa ameugua kwa muda mrefu, amekuwa akipatiwa matibabu tangu tarehe 14 Januari 2022 katika hospitali ya JKCI na baadae Afrika kusini na kurejea JKCI.

“Rais Samia anatoa polea kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu mkubwa. Pia, ametangaza siku tano za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa na serikali,” amesema Dk. Mpango.

Lowassa ni nani?

Edward Ngoyayi Lowassa ni mwanasiasa, mfugaji na mfanyabiashara aliyezaliwa tarehe 26 Agosti 1953.

Lowassa alianza masomo ya shule ya msingi huko Monduli tarehe 6 Januari 1961 na kuhitimu masomo yake mwaka 1967 kisha kujiunga na Shule ya Sekondari ya Arusha mwaka 1968.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1971 alijiunga na masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1972 katika shule ya vipaji maalumu ya Tabora na kuhitimu mwaka 1973.

 

Baadaye mwaka 1974 alijiunga na Chuo kikuu Dar es Salaam akasomea shahada ya kwanza katika taaluma ya sanaa ya maonesho ambapo mwaka 1977 alihitimu akiwa ni muigizaji mzuri wa sanaa za majukwaani aliyepikwa kitaalamu kabisa.

Lowassa alijaribu, kwa miaka sita kusaka ajira au kujiajiri kupitia taaluma yake lakini kwa bahati mbaya soko la filamu na sanaa za maonesho lilikuwa duni nchini, hivyo mwaka 1983 aliamua kurudi masomoni kusaka fani nyingine ambapo mwaka 1984 alipata shahada ya pili katika sayansi ya maendeleo ya jamii kwenye Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.

Baada ya kuhitimu shahada ya pili, Lowassa alifanikiwa kupata kazi serikalini akihudumu nafasi ya Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (1989 – 1990) kabla ya kuibukia kwenye siasa.

Kisiasa

Kada huyo wa CCM alianza kuwika rasmi katika anga za siasa mwaka 1990 alipogombea na kushinda ubunge Jimbo la Monduli na alishikilia kiti hicho kwa miaka 20.

Mwaka 1990 uchaguzi wa mwisho wa chama kimoja Lowasa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano akichukua nafasi ya Luteni Lepilal Ole Moloimet baada ya jimbo la Uchaguzi la Longido kuanzishwa na kumshinda Dk Toure katika kinyanyang’anyiro cha ubunge.

Katika serikali na chama Lowassa ameshika nafasi za Waziri wa Ardhi na Makazi mwaka 1993 – 1995, Waziri wa Maji na Mifugo mwaka 2000 – 2005 na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 – 2008.

Maamuzi magumu, urais

Mwaka 1995 Lowassa aliamua kuingia katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Wakati huo Lowassa aliombwa na Umoja wa Vijana kupitia kikao cha Baraza Kuu la Taifa achukue fomu akiwa miongoni mwa wana CCM wanne ambao vijana waliamini wataweza kulisaidia Taifa kupiga hatua za haraka kuelekea maendeleo endelevu. Wengine waliokuwa wametajwa na UVCCM ni Salim Ahmed Salim, Lawrence Gama na Jaji mstaafu Mark Bomani.

Katika hatua ya kuchagua majina matatu kati ya majina 11 yaliyoomba nafasi hiyo, Lowassa akawa hakupendekezwa, lakini hakununa wala kususa bali aliamini kuwa mwanamapinduzi mwenzie Jakaya Mrisho Kikwete ataweza kutekeleza dhamira aliyokuwa nayo ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Katika uchaguzi huo, Benjamini Mkapa ndiye aliyeteuliwa kuwania nafasi hiyo ambayo alifanikiwa kuitetea hadi mwaka 2005.

Tarehe 7 Februari 2008 Lowassa alijiuzulu baada ya kutuhumiwa kuwa ameshiriki katika kashfa ya kuipa zabuni ya kuzalisha umeme kampuni isiyo na uwezo ya Richmond. Ni baada ya Kamati ya Bunge kuchunguza mkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya Richmond Development Company LLC kutoka Houston, Texas.

Kamati ya wabunge watano chini ya mwenyekiti Harrison Mwakyembe ilibaini mkataba huo ulikuwa wa hovyo kwani Richmond ilipewa kazi ya kuzalisha megawati 100 za umeme kila siku baada ya ukame wa mwaka 2006 uliopunguza uwezo wa Tanesco. Kamati ilibaini baada ya Richmond kushindwa kuzalisha umeme mkataba ulihamishiwa kinyemela kampuni ya Dowans.

Kamati ya Bunge ikaona ya kwamba Lowassa alishawishi azimio kuhusu mkataba na Richmond kwa kupuuza masharti ya kisheria na kinyume cha ushauri wa TANESCO.

Baada ya kujadiliwa kwa taarifa ya kamati kwenye Bunge, Lowassa alichukua maamuzi magumu ya kujiuzulu pamoja na Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi waliowahi kuwa mawaziri wa nishati. Hata hivyo Lowassa alikataa ya kwamba alikuwa na hatia yoyote bali alizingatia maelekezo ya serikali.

Aidha, mwaka 2014 Lowassa alisimamishwa na kamati kuu ya CCM baada ya kushtakiwa ya kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hicho.

Mei 2015 hatimaye alianzisha kampeni yake rasmi ya kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais lakini Kamati Kuu ya CCM ilimwondoa katika orodha ya majina yaliyopelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya uteuzi wa majina matatu ya kupelekwa mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama.

Lowassa alichukua maamuzi magumu ya kuondoka CCM tarehe 28 Julai 2015 na kujiunga rasmi na chama cha upinzani cha Chadema.

Siku chache baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema na baadaye akawa mgombea wa Umoja wa Vyama vya Upinzani (Ukawa) uchaguzi uliofanyika Oktoba 2015. Kwa mujibu Tume ya Uchaguzi ya Taifa alishindwa alipata asilimia 39.97 ya kura zote huku mshindi akiwa  mgombea wa CCM John Magufuli aliyepata asilimia 58.46.

Lowassa aliendelea kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema. Mwaka 2016 alitangaza ya kwamba hawezi kurudi kamwe CCM.

Hata hivyo, Januari 2018 alifanya mazungumzo marefu na Rais Magufuli kisha tarehe 1 Machi 2019 akachukua maamuzi magumu ya kurudi kwenye chama chake cha awali CCM.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwinyi aungana na Samia kuuaga mwili wa baba yake

Spread the loveRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

error: Content is protected !!