Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu: Mabeyo awataje waliotaka kuzuia urais wa Samia
Habari za SiasaTangulizi

Lissu: Mabeyo awataje waliotaka kuzuia urais wa Samia

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema
Spread the love

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amevunja ukimya kwa kumtaka aliyekuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Venance Mabeyo, kuwataja watu aliodai “walitaka kuvunja Katiba,” ili kumzuia Rais Samia Suluhu Hassan kurithi kiti cha urais. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI kwa njia ya simu katika mahojiano maalum kutokea Ubelgiji juzi, Lissu alisema, ni muhimu Mabeyo akataja wahusika, ili kuondoa sintofahamu iliyojitokeza, kutokana na kauli yake hiyo.

“Nani aliyetaka kuvunja Katiba na utaratibu wa kuapishwa kwa Rais? Ni Diwani Athuman? Ni IJP Simon Sirro au Mabeyo mwenyewe?” alihoji Lissu na kuongeza, “Ni muhimu akataja wahusika na kuweka ushahidi.”

Kuibuka kwa Lissu, kumtaka Mabeyo kujitokeza kutaja waliotaka kuvunja Katiba, ili kumzuia Rais Samia asirithi kiti cha urais baada ya kufariki dunia, John Magufuli, kumekuja takribani wiki tatu baada ya mkuu huyo wa majeshi mstaafu, kunukuliwa akisema, kulikuwa na ugumu wa kumwapisha rais mpya.

Rais Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Rais Samia aliyekuwa makamu wa rais wakati huo, aliapishwa kurithi wadhifa huo, 19 Machi.

Kwa mujibu wa Mabeyo, haikuwa kazi rahisi kuapishwa kwa Rais Samia, kutokana na vuta nikuvute iliyoibuliwa na baadhi ya vigogo waliotaka kupindisha Katiba.

Akijibu kauli hiyo ya Mabeyo, Lissu alisema, “…katika hali ya kawaida, wanaoweza kupindisha Katiba, huwa ni wanajeshi. Yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa majeshi.

“Ni vema akatuambia akina nani waliotaka kufanya hivyo. Vinginevyo, anatuacha kwenye giza na taarifa zake zinageuka kuwa stori za mitaani zisizo na ushahidi.”

Alipoelezwa kuwa Jenerali Mabeyo ni kiongozi mkubwa nchini na hivyo, hawezi kuibuka na jambo ambalo hana ushahidi nalo, Lissu alisema, “Mabeyo ni mstaafu. Ni mtu huru, anaweza kusema chochote hivi sasa.”

Aliongeza: “Tujiulize, kama kulikuwa na viongozi waliotaka kuvunja Katiba kwa nini Rais Samia aliendelea kuwa nao? Alikuwa na wakuu wa usalama na watendaji wakuu wengine waliokuwapo kwenye utawala wa Magufuli.”

Amewataja viongozi hao, kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; aliyekuwa mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS), Diwani Athumani na aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.

Wakati Lissu akidai kuwa Samia ameendelea kubakiza serikalini watendaji karibu wote waliokuwa katika serikali ya Magufuli, gazeti hili limebaini kuwa ni Majaliwa pekee aliyesalia kwenye wadhifa wake mpaka sasa.

Sirro aliondoka katika kiti chake, mwaka mmoja kabla ya kustaafu. Aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe. Naye Diwani aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu -Ikulu. Siku mbili baadaye, uteuzi wake ukatenguliwa.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Bashiru Ally, aliyeteuliwa na Magufuli kushika wadhifa huo, alikuwa kiongozi wa kwanza kung’olewa kwenye nafasi yake. Dk. Bashiru alihudumu kwenye nafasi hiyo kwa siku 38 baada ya kuteuliwa kuwa mbunge.

Mabeyo alisema, wakati Magufuli anafariki dunia yeye alikuwa na wakuu wenzake wawili wa vyombo vya ulinzi na usalama, ambao ni Diwani na Sirro.

Alisema, baada ya kujadiliana juu ya kifo hicho, walimfahamisha Dk. Bashiru na Majaliwa, ambao anasema, walikuwa mkoani Dodoma.

Hata hivyo, kauli ya Mabeyo ya kuwaita Bashiru na Majaliwa waliokuwa Dodoma na kumuacha makamu rais aliyekuwa Tanga, ambako ni karibu zaidi, kuliibua utata kuhusu jambo hilo.

Kwa mujibu wa Ibara ya 37 (5) ya Katiba, “endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobakia…”.

Katika mazungumzo yake na MwanaHALISI, Lissu alisema, suala nani atashika mikoba ya urais iwapo rais aliyekuwapo madarakani atafariki dunia, kujiuzulu au kutokuwa na uwezo wa kuendelea na majukumu yake kutokana na ugonjwa halijawahi kubishaniwa kwakuwa liko wazi ndani ya Katiba.

“Katiba haina ugomvi juu ya kubadilishana madaraka pale rais aliyepo anapoondoka katika mazingira hayo matatu,” ameeleza.

Anasema, “Alichokisema Mabeyo hakina uhusiano na matatizo ya Katiba tuliyonayo. Inawezekana mstaafu huyo alisema hivyo kwa lengo la kuua baadhi ya ajenda au mijadala ya kitaifa iliyokuwa ikiendelea.

“Mimi nimeipokea kauli yake kwa tahadhari sana. Najua yawezekana aliisema kwa lengo la kumpamba Rais ili ionekane wao walikuwa imara kulinda Katiba na kuhakikisha anaapishwa,” ameeleza.

Lissu anasema, tatizo kubwa tulilonalo katika Katiba, ni kutoweka wazi namna ya kubadilisha madaraka pale inapotokea chama tawala kinashindwa uchaguzi.

“Tuna shida kubwa sana katika eneo hili. Ikitokea rais aliyepo madarakani akashindwa na upinzani, Katiba inataka akabidhi madaraka ndani ya siku saba kwa mshindi wa uchaguzi.

“Lakini Katiba haisemi atakabidhi kitu gani. Haisemi mawaziri atakaowachagua, watakabidhiwa nini. Haisemi makabidhiano kati ya chama kinachoondoka madarakani na kile kinachoingia, jinsi watakavyokabidhiana. Katiba imekuwa kimya katika eneo hilo,” ameeleza mwanasiasa huyo ambaye ni mwanasheria.

Anasema, “Katiba inasema rais atateua waziri mkuu kutoka chama chenye wabunge wengi. Ikiwa rais atakosa wabunge wa kutosha, atawezaje kuteua mawaziri wakati hawatoki kwenye chama chake?”

Alisema: “Haya ndiyo mambo tunayopaswa kuyajadili na kuyafanyia marekebisho, kwani siku ikitokea chama kilichoko madarakani kikashindwa uchaguzi, basi kutatokea mtafaruku mkubwa wa kikatiba. Kuna maswali mengi ambayo Katiba haina majibu yake. Tuachane na mambo madogo yanayosemwa na kina Mabeyo waliostaafu.”

Akifafanua zaidi, Lissu anasema, kwa mujibu wa Katiba iliyopo, rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali. Waziri mkuu ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni na katika Baraza la Mawaziri, ni mshauri tu wa rais.

Anasema: “Sasa Katiba inalipa Bunge mamlaka ya kumwajibisha waziri mkuu, kwa mambo yaliyoamriwa kwenye baraza la mawaziri, ambalo yeye si kiongozi wake. Mwenyekiti wa baraza la mawaziri ni rais. Huyu waziri mkuu, nje ya Bunge, ni waziri wa kawaida. Hana mamlaka yoyote. Anawajibishwaje katika jambo ambalo si lake (mwamuzi ni rais)?

“Mfano mzuri ni suala la mkataba wa Richmond, ambapo Bunge lilimshinikiza aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu wakati suala hilo, liliamriwa kwenye baraza la mawaziri lililokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete.”

Kifo cha Magufuli:

Mara baada ya kifo cha Magufuli, taarifa zinasema, baadhi ya vigogo waandamizi serikalini, walitaka Samia aliyekuwa kikazi mkoani Tanga, asirithi nafasi hiyo.

Badala yake, vigogo hao walitaka taifa lirejee kwenye uchaguzi wa rais, ambao tayari ulikuwa umefanyika miezi mitano iliyopita.

Waliotaka Samia asiwe rais, walishapiga hesabu Magufuli angeondoka 2025 na wao kupata fursa ya kugombea kiti hicho au kuweka mtu wao,” kimeeleza chanzo kimoja cha taarifa kutoka serikalini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!