December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kwaheri Dk. Shika

Spread the love

DAKTARI Luis Shika, aliyepata umaarufu kutokana na kauli yake ya ‘900 itapendeza,’ amehitimisha safari yake hapa duniani kwa mwili wake kuzikwa jana Jumanne tarehe 25 Agosti 2020 katika makaburi yaliyopo Kijiji cha Chamuda, Magu mkoani Mwanza. Anaripoti Brightness Boaz…(endelea).

Dk. Shika (70) alifikishwa Hospitali ya Nyanguge iliyopo Mwanza tarehe 22 Agosti 2020, kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Figo, hata hivyo, siku moja baadaye (23 Agosti 2020) alifariki dunia.

Umaarufu wa Dk. Shika nchini ulianzia kwenye mnada wa nyumba za Bilionea maarufu nchini Tanzania, Said Lugumi tarehe 9 Novemba 2017, baada ya kutangaza dau la juu ‘900 itapendeza.’

Mnada huo uliofanyika Mbweni na Upanga, ulisimamiwa na kampuni maarufu ya udalali ya Yono Auction Mart. Hata hivyo, Dk. Shika alishindwa kulipa fedha hizo na kusababisha sintofahamu jambo lililolazimisha mnada huo kurudiwa.

Kwenye mazishi yake, wasifu wa Dk. Shika umeeleza kwamba alizaliwa katika Kijiji cha Changasa mwaka 1950. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Changasa, baadaye alikwenda kusoma katika Shule ya Sekondari Musoma Alliance.

Dk. Shika alipata mafunzo ya uganga katika Chuo cha Waganga Wasaidizi mkoani Mbeya mwaka 1984 na mwaka 1991 alipata ufadhili na kwenda kusomea udaktari nchini Urusi.

Mwaka 1994, Dk. Shika alikwenda tena Urusi kusomea Shahada ya Uzamili wa magonjwa ya kuambukizwa na baadaye alisomea udaktari bingwa wa magonjwa ya akili.

Aliporejea nchini Tanzania, Dk. Shika alifanya kazi kama Mganga Msaidizi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, baadaye alikwenda tena Urusi kufundisha katika vyuo mbalimbali vya tiba.

Pia, Dk. Shika alianzisha biashara mbalimbali ikiwa ni pamoja kufungua Kampuni ya Lastford ya kusambaza kemikali viwandani nchini Urusi.

error: Content is protected !!