Saturday , 20 April 2024
Habari za Siasa

Urais waivuruga CCK

David Mwaijojele, Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK) wakati akipokea fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea urais wa Tanzania kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage
Spread the love

HATUA ya David Mwaijojele, Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK) kurejesha fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akiwa peke yake, imefukua mgogoro uliokuwa ukifukuta chini kwa chini ndani ya chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ikiwa ni siku moja baada ya Mwaijojele kurejesha fomu za kugombea urais wa Tanzania kupitia CCK akiwa peke yake Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma, viongozi wa chama hicho sasa wanavutana mashati.

Jana Jumanne tarehe 25 Agosti 2020, Katibu wa NEC, Dk. Willson Mahera alisema, baadhi ya masharti aliyoshindwa kukidhi wagombea hao wa CCK ni kutojazwa fomu namba 10 ya mgombea mwenza na picha za mgombea mwenza kutokuwepo.

Mwaijojele ambaye ni Mwenyekiti wa CCK Taifa, awali alivyokwenda kuchukua fomu pasi na mgombea wake mwenza, Ally Said Juma na viongozi wengine, pia alirejesha fomu hizo akiwa peke yake.

Hatua ya Mwaijojele kurejesha fomu akiwa peke yake, imemkasirisha Renatus Muabhi, Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye ameahidi kumchukulia hatua ‘mgombea’ huyo.

Renatus Muabhi

Akizungumza na MwanaHALISI Online leo Jumatano tarehe 26 Agosti 2020, Muabhi amemtuhumu Mwaijojele kulibeba sauala la kugombea urais yeye binafsi na familia yake.

“Kilichotoka jana ni madhira makubwa kwa chama na udhalilishaji mkubwa kwa chama chetu.”

“Mimi kama kiongozi mkuu wa chama, ule mchakato wa kumpata mgombea urais ulikuwa ni feki na haukubarikiwa. Mazingira hayo yalichangiwa na msajili,” amesema Muabhi.

Amesema, awali alieleza kuwa CCK hakikuwa na mazingira mazuri ya kusimamisha mgombea urais na kwamba mwenyekiti Mwaijojele alilazimisha hilo na akalifanya kwa pupa bila kushirikisha wengine.

“Mimi kama kiongozi wa chama, tuliona siyo sahihi na tukaona wacha tumwache aangalie mwisho itakuwaje. Kwa sababu hakuwa na ushirikiano na wengine, amejikuta anakwenda kuchukua fomu mwenyewe na amerejesha mweneywe,” amesema.

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Kutokana na hicho kilichotokea, Muabhi amesema “tunakwenda kulianglia hilo kwenye vikao, pia kuhoji ni kwa nini madhira haya yametokea, aeleze kwa nini ameweza kushindwa kuipigania nafasi ambayo siyo halali.”

Muabhi amesema, Mwaijojela amekiweka chama hicho kwenye sintofahamu ikiwa ni pamoja na hatari ya kupoteza uanachama na wanachama.

“Amekiweka chama katika mazingira hayo, unaweza kupoteza uanachama. Hivi mwenyekiti wa chama, anawezaje kwenda kugombea nafasi kama hiyo bila hata kulipia fomu, bila mgombea mwenza kukamiliha taratibu zake. Tukikutana katika vikao tutaona anachukuliwa hatua gani,” amesema.

Hata hivyo, Mwaijojele akizungumza na MwanaHALISI Online amejigamba kwamba, Muabhi hana uwezo wa kumchukulia hatua yoyote kwa kuwa si Katibu Mkuu wa chama hicho.

Kwenye maelezo yake (Mwaijojela) ameeleza kusikitishwa na kile alichoeleza kusalitiwa na mgombea mwenza wake Juma.

“Kwanza huyo uliyezungumza naye (Muabhi) siyo Katibu Mkuu wa CCK tangu 18 Julai 2020,” amesema Mwaijojela

Alipoulizwa sababu za kumwengua kwenye nafasi hiyo, Mwaijojele hakufafanua na badala yake alimjibu mwandishi ‘mambo yetu ya chama wewe hayakuhusu.”

Amesema, anayekaimu nafasi hiyo tangu tarehe 18 Julai 2020 ni Masoud Abadallah ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar.

Akijibu sababu za kutoambatana na mgombea mwenza katika Ofisi za NEC wakati wa kurejesha fomu jana tarehe 25 Agosti 2020, amedai mgombea huyo (Ally Said Juma) alikuwa na dharura.

Amsema, yeye na mgombea mwenza walishirikiana katika kutafuta wadhamini, hata hivyo amedai “kuna hila zimetumika kumkwamisha mgombea mwenza wangu.”

Masoud Abdallah, anayetajwa kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho akizungumza na mtandao huu amedai, tarehe 18 Julai 2020 Kikao cha Kamati Kuu alichokiendesha yeye mwenyewe, kilimvua uongozi Muabhi.

Dk. Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC

Amesema, wajumbe wa kikao hicho ni 26 lakini waliohudhuria walikuwa 16, hivyo akidi ya kufanya uamuziwa kumtimua ilitimia.

“Yeye Muabhi alisema, mbona wajumbe waliohudhuria hawajui, sisi tukasema ni halali na kama uamuzi tuliouchukua hakuridhika, aende kwa msajili,” amesema Abdallah.

Amesema, suala la kumvua uongozi Muabhi halifahamiki kwa sababu baada ya kumalizika kwa kikao hawakufanya kikao na waandishi wa habari jambo ambalo limewafanya hata baadhi ya wanachama wao kutokufahamu.

Akieleza sababu za kutomsindikiza mgombea urais wa chama chake NEC, amesema “nikiwa bandarini Zanzibar kwa safari ya Dodoma, nilipata kizungumzu juzi na nilizinduka jana saa 9. Hivyo nilitamani kuhudhuria ili ndiyo hayo matatizo niliyopata.”

Akizungumzia kutoonekana kwa mgombea mwenza kwenye ofisi za NEC amesema, “mgombea mwenza, sitaweza kulijibu kwani tangu mwanzo alikuwa na matatizo makubwa sana na tulitarajia muda ukifika liwe limemalizika.”

Hata hivyo, amesema, Novemba 2020 anatarajia kuitisha kikao kwa lengo la kujadili mienendo ya chama hicho.

MwanaHALISI Online limemtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ambaye amesema, chama hicho kilifanya mabadiliko ya viongozi na kuwa, Muabhi si Katibu Mkuu wa CCK. Hata hivyo, ameeleza kutokuwa tayari kuzungumzia zaidi suala hilo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Mtandao huu umezungumza na Richard Kiyabo, Makamu Mwenyekiti wa CCK – Bara ambaye amesema, “hili suala (la Muabhi) lilifanyika kimakosa na mahakama haijathibitisha kwamba alikutwa na rushwa.”

Kiyabo amesema, kushikwa na rushwa ni jambo moja na kukutwa na hatia ni jambo jingine.

“Suala la kuondolewa, Kamati Kuu na Mkutano Mkuu ndiyo inaweza kumwondoa kwenye uongozi. Alichaguliwa na mkutano mkuu wa chama na huo mkutano mkuu ndiyo ulitakiwa kumwondoa,” amesema Kiyabo na kuongeza:

“Lakini Wajumbe wa Mkutano Mkuu halisi hawajaitwa, ni watu tu fulani walichukuliwa na kuwekwa hapo ili wamwondoe mtu aliyechaguliwa na Mkutano Mkuu, kwa hiyo hilo siwezi kulisemea kwamba aliondolewa na mimi sikuwepo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!