ABDULRAHMAN Kinana, Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameonesha hofu ya kuanguka kwa chama hicho endapo wanachama wake watapuuza kupiga kura. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bagamoyo … (endelea).
Amesema, baadhi ya wanachama wa chama hicho wamekuwa wakisema kwamba mgombea wao urais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ‘atapita tu’ na hivyo kupuuza kwenda kupiga kura.
“Hatari ninayoiona ni kuwa, wengi wanasema si atapita tu, ninachowasihi kupita kwake ni kwenda kumpigia kura. msiridhike na hali iliyopo kwamba anakubalika mgombea wetu wa urais,” amesema Kinana.
Ametoa kauli hiyo jana Jumatatu tarehe 31 Agosti 2020, akiwa Miono uliopo Halmashauri ya Chalinze, Bagamoyo Mkoa wa Pwani wakati akizindua kampeni za chama hicho akimnadi Ridhwan Kikwete (Jimbo la Chalinze) na Mwarami Mkenge (Bagamoyo) na madiwani wa chama hicho.
Alisema, wanachama wa chama hicho, wanapaswa kujiandaa na kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba 2020.

Na kwamba, chama hicho ili kushinda kinategemea kwa kiwango kikubwa kujitokeza kwa wanachama wao kwenda kupiga kura.
“Tegemeo letu kubwa ni wanachama wa CCM kuhamasisha wananchi ili siku ya uchaguzi, waende kupiga kura tufanikishe ushindi wa kishindo kuanzia rais, wabunge na madiwani.”
“Tegemeo letu wanachama wa CCM, tunawategemea mabalozi, viongozi wa kata na ngazi zote kuhamasisha wananchi kwenda kupiga kura, kampeni ni muhimu, lakini lazima tujipange vizuri kwenda kupiga kura,” alisema.
Kwenye kampeni hizo, Kinana alimtaja Dk. Magufuli kwamba ni kati ya viongozi wenye ujasiri, mwadilifu jambo ambalo limeshuhudiwa na Watanzania wengi.
Kinana amewasihi wananchi kuchagua wagombea waliosimamishwa na chama hicho ili wakaungane na Dk. Magufuli katika kupeleka zaidi mbele maendeleo.
Leave a comment