April 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wizara ya Elimu Tanzania yatoa maagizo vyuo vya maendeleo 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. AveMaria Semakafu (katikati) akizungumza na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same.

Spread the love

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, imevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kujikita kutoa mafunzo ya fani zinazopendwa na zinazotoa ajira badala ya kuendelea kuwa na fani ambazo hazina wanafunzi katika eneo husika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Hayo yamesemwa jana Jumatatu tarehe 31 Agosti 2020 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. AveMaria Semakafu alipofanya ziara ya kukagua ukarabati na uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same mkoani Kilimanjaro.

Dk. Semakafu alisema ni vizuri vyuo vikajiimarisha kwenye utoaji mafunzo kwa fani zenye wanafunzi  wengi na kuachana na zile zenye wanafunzi wachache.

“Kuanzia mwaka huu, kila chuo cha wananchi kitafundisha fani ambazo zinahitajika katika maeneo husika kwa maana ya kuwa na wanafunzi wa kutosha, hakuna chuo chochote kusajili fani ambazo zina wanafunzi wachache ama chini ya 12.”

“Serikali haiajiri walimu kufundisha wanafunzi wawili hivyo hakuna haja ya kuweka fani ambazo hazina wanafunzi wa kutosha,” alisema Dk. Semakafu.

Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same

Alisema mpango wa ‘Elimu haina mwisho’ unaotolewa katika vyuo hivyo ni utaratibu wa kutoa fursa kwa watoto waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii ili kuwasaidia kupata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuendelea na masomo na kuendesha maisha yao pindi watakapohitimu hivyo wanapaswa kufundishwa kama wanafunzi wengine bila kuwatenga.

Alisema, Serikali iliamua watoto hao wasome katika vyuo hivyo kupitia mfumo usio rasmi bila malipo yoyote kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa nyingine ya kuendelea na masomo na kuutaka Uongozi wa chuo cha Maendeleo Same  kuwarudisha chuoni wanafunzi wote walioacha masomo kwa sababu mbalimbali ili waweze kumaliza masomo yao.

“Tumeanza programu hii kwa lengo la kupata watoto wote walioacha shule na ndio maana unaona hata wasichana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali tumewarudisha katika mfumo huu ili waje waendelee na masomo na na wale wenye watoto hata tuna shule za chekechea kwa ajili ya watoto wao,” alisema Dkt. Semakafu.

Dk. Semakafu alikagua miundombinu iliyokarabatiwa na kuboreshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo aliuagiza uongozi wa chuo hicho kufanya marekebisho katika baadhi ya miundombinu ambayo haikukarabatiwa vizuri.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same, Edward Mdee  aliishukuru wizara kwa ukarabati ambao umefanyika chuoni hapo, na kusema kuwa chuo hicho chenye wanafunzi 301 kipo katika mkakati wa kuboresha utoaji wa mafunzo ili kuhakikisha kinatoa vijana wenye ujuzi na maarifa yatakayowawezesha vijana wa Same kujiajiri ama kuajiriwa.

error: Content is protected !!