May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kada wa Chadema’ akabidhiwa na CCM kuongoza Kamati ya Bunge ya PAC

Naghenjwa Kaboyoka

Spread the love

HATIMAYE Naghenjwa Kaboyoka, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amerejeshwa tena kuongoza nafasi hiyo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kaboyoka aliyepata kuwa mwenyekiti wa kamati ya PAC, katika Bunge lililopita, alitangazwa kuongoza tena nafasi hiyo jana, Jumatatu, mjini Dodoma.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Kaboyoka alituhumiwa na baadhi ya wabunge wenzake wa Chadema na Ukawa, kutowapa ushirikiano; akidaiwa kufanya kazi zaidi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Spika na mawaziri.

Vyanzo vya taarifa vilisema, baadhi ya wabunge wenzake wa upinzani, walimtuhumu Kaboyoka kuwa ni mmoja wa wabunge wa upinzani, waliokuwa wanasaidia serikali, kuficha walichoita, “maovu yake.”

          Soma zaidi:-

Mwanasiasa huyo aliyepata kuwa mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, katika jimbo la Same Mashariki, kati ya Novemba mwaka 2015 na Agosti mwaka jana, ni miongoni mwa waliokuwa wanachama 19 wa Chadema, waliovuliwa uanachama.

Kaboyoka na wenzake wengine 18, akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima James Mdee, walitangazwa kuvuliwa uanachama wa chama hicho, tarehe tarehe 27 Novemba mwaka jana.

Walituhumiwa na kupatikana na makosa ya utovu wa nidhamu na usaliti; kughushi nyaraka za chama, upendeleo, kuhujumu chama, kutengeneza migogoro; kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe.

Hata hivyo, maamuzi hayo ya Chadema yaliyofanywa na Kamati Kuu (CC), yalipingwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa madai kuwa “watuhumiwa hawakusikilizwa.”

Spika Ndugai alinukuliwa na vyombo vya habari, tarehe 8 Desemba 2020, akieleza kuwa hatambui maamuzi hayo ya CC na kuongeza, “kama Chadema hakitaki Mdee na wenzake kuwa wabunge, basi kiende Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) au mahakamani.”

Alitoa kauli hiyo, wakati wa kuwaapisha wabunge wawili walioteuliwa na Rais John Magufuli, kuwa wabunge na mawaziri – Dk. Dorothy Gwajima na Dk. Leonard Chamriho.

Kamati Kuu ya Chadema, iliyokutana chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, tarehe 27 Novemba 2020, iliamua kwa kauli moja, kumuondoa Mdee kwenye nafasi yake ya uenyekiti wa Bawacha na kisha kumfuta uanachama.

Kaboyoka, Mdee na wenzake, ambao wamepachikwa jina la Covid 19 na wanachama na viongozi wa Chadema, wamewasilisha rufaa zao Baraza Kuu (BKT), kupinga maamuzi ya kuwafuta uanachama.

Wengine waliofutwa uwanachama, ni pamoja na waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega na mwenzake wa Baraza la Vijana Bavicha, Nusrat Hanje.

Wengine, ni aliyekuwa makamu mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga; aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliokuwamo katika orodha hiyo, ni aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed; aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Arusha, Ceciia Pareso; aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda na aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dodoma, Kunti Majala.

Yumo pia, aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba; aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es Salaam,   Anatropia Theonest, aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Kagera, Conchesta Lwamlaza; na waliokuwa wanachama wengine  wawili, Felister Njau na Stella Siyao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Chadema, uteuzi wa Kaboyoka katika wadhifa huo, ni miongoni mwa mambo ambayo Mdee na viongozi wenzake waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanakuwa wabunge, “walikubaliana na baadhi ya watu waliowasaidia kupata ubunge.”

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online anasema, “Kaboyoka hakuwamo kwenye orodha ya kwanza iliyoandaliwa na akina Mdee iliyokwenda NEC. Jina lake, liliingizwa baada ya kupewa masharti ya kufanya hivyo.”

Anasema, “watu ambao walisaidia kina Mdee kuwa wabunge, bila idhini ya chama, ndio waliomfanya Kaboyoka kuwa mbunge.” Orodha hiyo ya awali, iliyoandaliwa na Mdee na mwenzake Tendega, iliyopelekwa NEC, ilikuwa na majina wanachama 37 wa chama hicho.

Kuhusu madai kuwa katika Bunge lililopita, ambako Kaboyoka alikuwa mwenyekiti wa PAC na hivyo hakuweza kusaidia taifa na upinzani kwa ujumla, mtoa taarifa huyo anasema, “kuna wakati, tulipendekeza kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, kumuondoa katika nafasi ya uyenyekiti.”

Anaongeza, “kwa kweli, Kaboyoka hakuwa na msaada kwa Chadema, wananchi waliokuwa wanataka usimamizi mzuri wa rasimali zao, wala nchi wahisani zinazochangia bajeti ya maendeleo.”

“…kwa bahati mbaya, pendekezo letu, halikufanyiwa kazi. Alikuwa mbunge wa Chadema, aliyekuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi, na tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, mambo mengi yaliyokwenda bungeni, yalihaririwa kwa kiwango kikubwa.”
Anasema, Mdee alikuwapo bungeni wakati Kaboyoka akituhumiwa kutofanya kazi zake ipasavyo, na alikuwa mmoja wa watu ambao walimlalamikia kusaidia serikali kuficha maovu yake.
Amesema, “Mdee anajua hili na hivyo kama kweli hawa watu wangekuwa wamekwenda bungeni kwa maslahi ya Chadema, kama ambavyo wamekuwa wakieleza, basi wasingeruhusu Kaboyoka kuwa mwenyekiti wa PAC. Lakini kwa kuwa kuingia kwao bungeni, ni mkakati maalum wa kuisafisha serikali, kufuatia yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu uliyopita, ndio maana haya yametokea.”

Miongoni mwa mambo ambayo Kaboyoka alidaiwa kuyamazia, ni pamoja na sakata maarufu la Sh. 1.5 trilioni.

error: Content is protected !!