July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai awapiga ‘stop’ Chadema ‘nendeni NEC au mahakamani’              

Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge Tanzania

Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania, amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) au mahakamani, ili waliokuwa wanachama wake 19, wakiongozwa na Halima Mdee, waweze kuvuliwa ubunge. Anaripoti Brightness Boaz, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, “kuna mambo yanayoendelea, tuendelee kuangalia hiyo senema. Kwamba, spika unaambiwa wafukuze hao wabunge 19, najiuliza, niwafukuze kosa langu ni kuwaapisha?”

Ameongeza, “niwakumbushe ndugu zangu wa (Chadema), hili jambo kama linawalakini, ni muhimu kufuatilia NEC na mahakamani, lakini kuniambia mimi niwafukuze hiyo siyo kazi yangu.”

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo, leo Jumanne tarehe 8 Desemba 2020, wakati wa hafla ya kuwaapisha wabunge wa kuteuliwa na Rais John Magufuli, Dk. Dorothy Gwajima na Dk. Leonard Chamriho, iliyofanyika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

          Soma zaidi:-

Amesema, Chadema hakipaswi kumweleza yeye kuwachukulia hatua wabunge hao, ikiwamo kuwafukuza, badala yake akaelekeza chama hicho kupeleka malalamiko yake, NEC na mahakamani.

Hata hivyo, wakati Ndugai anaitaka Chadema kuwasilisha malalamiko yake NEC au mahakamani, miaka mitatu iliyopita, alipokea na kuifanyia kazi barua iliyowasilishwa na Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) kumtaarifu wabunge nane wa viti maalum kutoka chama hicho, wamefutiwa uanachama wao.

Katika barua hiyo ya tarehe 26 Julai 2017, Spika Ndugai alisema, ameridhia uamuzi wa Prof. Lipumba kuwafutia uanachama wabunge hao, kwa tuhuma za kinidhamu, kukihujumu chama, kumkashifu na kumdhalilisha Prof. Lipumba.

Alisema, amejiridhisha kuwa wabunge hao wamefutiwa uanachama wao kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo hawana sifa za kuendelea na Ubunge.

Akasema, kwa mamlaka aliyonayo kwa kuzingatia kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kikisomwa pamoja na kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, alitangza nafasi hizo kuwa wazi na akaitaarifu NEC kuendelea na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa sheria.

Waliovuliwa ubunge, walikuwa ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mohemed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally al Kassmy na Halima Ali Mohamed.

Aidha, ni Ndugai aliyeridhia hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumfutia uanachama aliyekuwa mwenyekiti wake wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, hatua ambayo ilimsababisha kupoteza ubunge wake.

Taarifa zinasema, kilichotokea kwa Mdee na wenzake 18, kinafanana na kilichompata Sophia Simba. Kwamba, tarehe 11 Machi 2017, alifutwa uanachama na chama chake kwa tuhuma za usaliti na CCM kikamwandikia barua Spika Ndugai kumtaarifu uamuzi huo.

Baada ya barua hiyo, Spika Ndugai aliiandikia NEC barua ya kuwajulisha uamuzi huo na hivyo, NEC ikatangaza jina la mwanachama mwingine wa chama hicho kuwa mbunge wa Viti Maalum.

Naye Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, mara baada ya kupokea barua ya Spika Ndugai, tarehe 12 Aprili 2017, aliufahamisha umma juu ya barua aliyoipokea kutoka kwa Spika Ndugai kuhusiana na kiti hicho kuwa wazi.

Alisema, taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa uanachama wa Chadema kwa tuhuma za usaliti, kughushi nyaraka na kujipeleka bungeni kuapishwa Spika Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, huku wakijua kuwa chama hicho, hakijapendekeza majina ya wabunge wake NEC.

Katika kikao chake cha Kamati Kuu (CC), kilichokutana chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, tarehe 27 Novemba 2020, kulitangazwa kuwa Mdee na wenzake wamevuliwa nafasi zao zote za uongozi na uanachama wa chama hicho.

Chadema kimesema, iwapo watuhumiwa hao 19, waliopachikwa jina la Covid 19, hawakuridhika na hatua hiyo, basi wanaweza kukata rufaa Baraza Kuu (BKT), ndani ya siku 30 tangu kutolewa uamuzi huo.

Barua kutoka Chadema kwenda kwa Spika Ndugai, imesainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.

Wengine, ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha Bara, Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Katika orodha hiyo, yupo pia aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum katika Bunge lililopita, kutoka mkoani Arusha, Ceciia Pareso; aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki,  Naghenjwa Kaboyoka; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Mbeya, Sophia Mwakagenda na aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Dodoma, Kunti Majala.

Wengine, ni aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Shinyanga, Salome Makamba; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Dar es Salaam,  Anatropia Theonest; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Kagera,  Conchesta Lwamlaza; na wanachama wengine wawili, Felister Njau na Stella Siyao.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM, (UWT), Sophia Simba (kushoto) akiwa na Rais Jakaya Kikwete

Kama vile alikuwa anajibu barua hiyo ya Chadema, Ndugai alisema, kuna njia mbili za yeye kupata majina ya wabunge wanaopaswa kuapishwa.

Amezitaja njia hizo kuwa NEC kumwandikia barua yeye na kisha majina yao kutangazwa kwenye gazeti la serikali, akisisitiza kuwa  “utaratibu wote huo ulizingatiwa.”

Kabla ya kujibu barua ya Mnyika, Spika Ndugai aliwakaribisha bungeni, Dk. Dorothy na Dk. Chamriho na kuwaeleza kuwa Bunge litawapa ushirikiano wa kutosha ili kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Mbali na kuwateua kuwa wabunge, Rais Magufuli alimteua Dk. Dorothy kuwa waziri wa afya na Dk. Chamriho kuwa waziri wa ujenzi na uchukuzi.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Dorothy alikuwa naibu katibu mkuu, Ofisi ya Rais-Tamisemi anayeshughulikia afya huku Dk. Chamriho akiwa katibu mkuu- uchukuzi.

Naye Dk. Dorothy akizungumza mara baada ya kuapishwa alisema, “natambua kazi iliyoko mbele ni kubwa na inahitaji uzalendo, ujasiri na ushirikiano.”

Alisema, amini kabisa kuwa rais yupo, Bunge lipo, Chama Cha Mapinduzi kipo na wananchi wapo na katika yote anaamini yeye kama mama, mke, kwamba familia yake ipo pamoja naye.

Kwa upande wake, Dk. Chamriho amesema, “haya majukumu tuliyokabidhiwa ni magumu na mazito. Tunaomba kwa umoja wenu ushirikiano na kuombeana ili tuweze kukamilisha yote na kuitimiza ndoto za huyo aliyetuamini na hata kutupatia madaraka haya.”

Amesema, “ninaahidi nitafuata yale nitakayopangiwa na ninaomba mheshimiwa Spika, mnipokee katika majukumu haya mapya.”

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa kumwapisha Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais.

Amesema, “…uapisho ule unathibitisha alichozungumza Rais John Magufuli alipokuwa anaapishwa (5 Novemba 2020) kuwa sasa uchaguzi umekwisha na kutokana na kuisha kwa uchaguzi huo, ndiyo haya mnayoyaona.”

Amesema, serikali inazidi kuundwa na kule Zanzibar, Baraza la Wawakilishi linafanya kazi. Makamu wa Rais, Maalim Seif ameapishwa, “na kesho tutashuhudia mawaziri wakiapishwa.”

error: Content is protected !!