Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Joseph Selasini, wenzake 8 wapigwa ‘Stop’ NCCR- Mageuzi
Habari za SiasaTangulizi

Joseph Selasini, wenzake 8 wapigwa ‘Stop’ NCCR- Mageuzi

Spread the love

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewazuia “viongozi” tisa wa NCCR- Mageuzi, kutojihusisha na uendeshaji wa shughuli ndani ya chama hicho. Anaripoti Faki Sosi na Juliana Assenga (UDSM) …(endelea).

Miongoni mwa waliyokatazwa, ni pamoja na kuratibu, kuendesha na kusimamia vikao vya Sektarieri, Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na mkutano mkuu wa chama hicho.

Waliosimamishwa na Mahakama kujihusisha na masuala ya ndani ya NCCR- Mageuzi, ni Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Haji Ambari Khamisi; aliyekuwa Katibu Mkuu, Martha Chiomba na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Ameir Mshindani Ali.

Baadhi ya wanachama wa NCCR Mageuzi wakiwa katika viunga vya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.

Wengine, ni Susanne Masele, Mweka Hazina taifa; Joseph Roman Selasini, aliyekuwa mjumbe wa NEC; Beati Mpitabakana, Martin Mng’ong’o, Ramadhan Manyeko na Hassan Ruhwanya.

Mdawa mwingine kwenye kesi, ni Bodi ya Wadhamini ya chama hicho (Registered Trustees of NCCR-Mageuzi.

Uamuzi huo umetolewa leo tarehe 7 Septemba, 2022 mahakamani hapo, kufuatia ombi lililowasilishwa na Makamu mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi (Bara), Angelina Mutahiwa na mjumbe wa NEC, Hemedi Kanoni.

Wadai hao wawili, wanawatuhumu wadaiwa kuwa wanakula njama za kutaka “kukivuruga” chama hicho “kwa manufaa yao binafsi.”

Mapema asubuhi, Jaji wa Mahakama hiyo, Edwin Kakolaki, alisikiliza hoja za mawakili wa waleta maombi, wakiongozwa na Juma Nassor, likiwamo la kutaka kuzuiwa kwa vikao vyote vinavyoratibiwa na genge hilo.

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi

Kupitia wakili wao, waleta maombi waliiambia Mahakama madhara lukuki ya kutotolewa kwa zuio hilo, pamoja na kuiomba Mahakama itangaze kuwa unaoitwa “mkutano wa NEC,” wa tarehe 21 Mei 2022, ulikuwa batili.

Mkutano huo, ulifanyika katika ukumbi wa Salvation Army, jijini Dar es Salaam na kuishia kumuondoa kwenye wadhifa wake, mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na wenzake kadhaa.

Ni kupitia mkutano huo, Selasini ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Rombo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alijitangaza kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na Katibu Mwenezi wa chama hicho.

Shauri hilo la madai lilifunguliwa mahakamani hapo juzi Jumatatu kwa hati ya dharura na kupewa Na. 150/2022.

Aidha, waleta maombi wameitaka Mahakama kutamka kuwa wadaiwa hawana mamlaka ya kikatiba ya kuitisha vikao vya Sekretieti, kamati kuu, NEC na mkutano mkuu.

Wajibu maombi waliohudhuria mahakamani, ni Mpitabakana, Mng’ong’o mwenyekiti wa Bodi, Mohammed Tibanyendela na mjumbe wa bodi hiyo, Thomas Nguma.

“Mheshimiwa Jaji, maombi yameombwa chini ya hati ya dharura, kuna vikao vinaendelea leo, kesho, tarehe 8 na tarehe 15 ambavyo vitaathiri shauri hili. Tumeomba ziuo kwa wajibu maombi kutoendelea na vikao hivyo, mpaka maombi hayo yatakaposikilizwa na kuamriwa,” alieleza wakili Nassoro.

Alipoulizwa na Mahakama mjibu maombi namba tano, (Mpitabakana) endapo anakubaliana na ombi la waombaji la kuzuiwa kwa mikutano hiyo, alieleza kuwa hakubaliani nalo kwa kuwa shughuli za chama cha siasa zikizuiwa maendeleo ya chama yatadorora.

Joseph Selasini akikabidhiwa kadi ya NCCR- Mageuzi na James Mbatia pindi alipohamia ndani ya chama hicho kutoka Chadema.

Alisema, “chama ni vikao, kama kutakuwa hakuna vikao kitakuwa mfu huwezi kuamua jambo kama wewe Katibu Mkuu pekee yako lazima uite vikao.”

Naye Mng’ong’o aliimbia Mahakama, “mimi sijapokea wito wa kikao kwa tarehe hizo …wangesema wataathirika vipi wawasilishe ajenda ambayo wanaona wao kuwa itawaathiri ili isijadiliwe mpaka uamuzi.”

Kwa upande wake, Tibanyendela aliieleza Mahakama kuwa Bodi ya wadhamini imepata nyaraka za maombi hayo jana hivyo wanaomba muda wa kujibu maombi hayo.

“Mleta maombi namba moja namtambua ni Makamu Mwenyekiti Bara, hivyo vikao vinavyoombwa vizuiliwe ndivyo vilivyoleta mtafaruku ndani ya chama kuna vikao kadhaa ndivyo vilivyoleta mgogoro hivyo vikizuiwa havitakuwa na athari ndani ya chama tutajibu mapema ili shughuli za chama ziendelee,” alieleza.

Wakili Nassoro akijibu hoja za wajibu maombi namba tano na sita, alisema kuwa Mahakamani iwazuie wajibu maombi na mawakala wao, kushiriki na kuratibu mikutano yote ya chama hicho, ili kulinda hadhi ya waombaji.

“Nimeomba wajibu maombi namba moja mpaka tisa kuzuiwa kushiriki na kuitisha vikao, hakuna aliyetoa sababu za kwanini vikao hivyo visizuiliwe. Naomba Mahakama itukubalie ombi letu,” alisisitiza.

Edward Simbeye, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma

Aliongeza: “Kama Mahakama haitaweka zuio hilo, kutakuwa hakuna maana ya maombi haya kuwapo mahakamani.”

Katika uamuzi wake, Jaji Kakolaki alisema: “Mahama inakubaliana na hoja za waleta maombi na hivyo, inawazuia wadaiwa wa kwanza hadi tisa kuratibu mkutano wowote mpaka maombi hayo yatakaposikilizwa.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa 15 Septemba mwaka huu, ambapo 13 Septemba, wadaiwa watapaswa kuwasilisha kiapo kinzani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Spika Tulia aibana Serikali mafao ya wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Spread the loveSPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameitaka Serikali kufanya tathimini...

Habari za Siasa

Serikali yawapa maagizo Ma-RC udhibiti magonjwa yasiyoambukiza

Spread the loveWAKUU wa mikoa nchini wametakiwa kuandaa utaratibu wa kuwawezesha wananchi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

error: Content is protected !!