Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Jaji Biswalo aendelea kung’ang’aniwa fedha za ‘Plea Bargaining’, CUF wataka ajiuzulu
Habari za Siasa

Jaji Biswalo aendelea kung’ang’aniwa fedha za ‘Plea Bargaining’, CUF wataka ajiuzulu

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga
Spread the love

 

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, ajiuzulu cheo chake cha ujaji wa Mahakama Kuu, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za upotevu wa baadhi ya fedha zilizopatikana kupitia mchakato wa kisheria wa makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo tarehe 8 Februari 2023 na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, baada ya hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, kuiagiza tume aliyounda kuangalia namna ya kuboresha taasisi za haki jinai, ikafanye uchunguzi dhidi ya fedha hizo, kufuatia kuibuka madai ya kwamba baadhi yake zimefichwa katika akaunti za benki nchini China.

Prof. Lipumba amedai kuwa, ili uchunguzi huo ufanyike kwa haki, inabidi Jaji Biswalo na waliokuwa wasidizi wake wakati wa mchakato huo, wajiuzulu ili uchunguzi huo ufanyike kwa uhuru.

“Hata wale watumishi waliokuwa wakimsaidia Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kipindi hicho cha “Plea Bargaining” wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi huru wa tume hiyo na uchunguzi wake utakuwa wenye tija na kufuata utawala wa sheria pamoja na kurejesha imani ya Watanzania katika ofisi husika,” amesema Prof. Lipumba.

Mwanasiasa huyo amesema tume hiyo pia ichunguze kama kuna viongozi na taasisi nyingine zilizohusika katika sakata hilo, fedha zilizopokelewa taslimu na zilizowekwa kwenye akaunti za benki, pamoja na mali zisizohamishika zilizowekwa kama dhamana kwa wale walioshindwa kulipa fedha taslimu, kama bado ziko mikononi mwa Serikali au zimerejeshwa kinyemela.

“Wale watakaobainika wamehusika katika sakata hili ama la upotevu wa fedha au matumizi mabaya ya ofisi husika basi wachukuliwe hatua za kisheria ili kuzuia matukio kama haya kujirudia tena. Tuna matumaini tume itafanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, bila woga wala upendeleo na tunaitakia utekelezaji mwema wa majukumu yake,” amesema Prof. Lipumba.

Mbali na CUF, kuna baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo Chama cha ACT-Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), pamoja na watetezi wa haki za binadamu, katika nyakati tofauti walimtaka ajiuzulu kupisha uchunguzi dhidi ya fedha hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!