WAKILI Hekima Mwasipu na wenzake wawili, wamefungua kesi katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, kupinga masharti mapya yanayowalazimisha mawakili kuwa wanachama wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Leo tarehe 8 Februari 2023, kesi hiyo Na. 2/2023, kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo, mbele ya Jaji Moses Mzuna.
Jaji Mzuna alitoa amri kwa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na EALS, ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuwasilisha hati kinzani ndani ya siku 14 kuanzia leo, hadi tarehe 28 Februari 2023.
Baada ya kutoa amri hiyo, Jaji Mzuna aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 1 Machi mwaka huu, ambapo itakuja kutajwa tena.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Wakili wa waleta maombi, Selemani Matauka, amedai wateja wake wamefungua kesi hiyo kupinga sharti la wanachama wote wa TLS kuwa wanachama wa lazima wa EALS, ilhali taasisi hiyo ni kampuni binafsi.
Pia, wanapinga kipengele cha kutopewa vitambulisho vya uwakili vya uanachama wa TLS, hadi watakapolipa ada ya uanachama wa EALS, kiasi cha Dola za Marekani 20.
Mbali na Wakili Mwasipu, mawakili wengine waliofungua kesi hiyo ni, Frank Chundu na Deogratius Mahinyira.
Leave a comment