Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Hii ndio sura halisi ya Rais Samia
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hii ndio sura halisi ya Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

KILA zama na kitabu chake. Hizi ni zama za Rais Samia Suluhu Hassan na kitabu anachotumia ni tofauti na kilichotumiwa na mtangulizi wake hayati Dk. John Magufuli.

Kitabu anachotumia Rais Samia anajenga haiba yake kwa hulka ya upole; hatishi wasaidizi wake wala kuwafokea au kuwasuta hadharani. Ni mpole lakini msikivu, ni mchapakazi asiye na majivuno. Hana nongwa hata na wanaomkejeli, wanaokosoa au kumpinga.

Hayati Magufuli, katika awamu yake, aliainisha vipaumbele kadhaa kwa ajili ya kuinua uchumi ambao alidai ulikuwa chini kwa kuanzisha miradi ya kimkakati na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na kilimo.

Alisifiwa kwa hilo lakini aliharibu haiba yake mbele ya macho ya jamii kwa hulka yake ya kufoka, kukaripia watendaji hadharani, kuwaibisha na kuwatumbua wakati mwingine kwa makosa ya hisia tu.

Rais Samia amekuwa tofauti. Alipoingia Ikulu Machi 19, 2021, mbali ya kuweka vipaumbele ambavyo vimelenga kuwatoa Watanzania katika dimbwi la umasikini hasa sekta zinazowainua wengi ikiwamo ya kilimo yenye asilimia 70 ya Watanzania, pia amefanya maboresho katika utoaji huduma za jamii.

Staili yake ya upole iliwachanganya wengi katika kipindi cha miezi sita ya kwanza alipoingia na Baraza la Mawaziri aliloteua Machi 30, 2021.

Wananchi na watumishi kwa ujumla walikuwa wanajaribu ‘kujichekecha’ ili kuenenda na maono ya mkuu huyo wa nchi lakini naye alikuwa anawasoma.

“Kipindi cha miezi sita ya urais wangu nilikuwa najifunza. Katika uongozi kuna mbinu nyingi. Serikali yetu itaendeshwa na matendo makali na siyo maneno makali; matendo makali si kupigana mikwaju bali ni kwenda kwa wananchi kutoa huduma inayotakiwa kila mtu kutimiza wajibu wake,” alisema.

Samia Septemba 13, 2021 alipokuwa akiwaapisha baadhi ya mawaziri kutokana na mabadiliko ya kwanza ya baraza lake la mawaziri.

“Msitegemee kwa maumbile yangu haya, pengine na malezi yangu, msitegemee kukaa hapa nianze kufoka. Nahisi siyo heshima. Kwa sababu nafanya kazi na watu wazima naamini wanajua wanachokifanya; sitokaa nikaanza kufoka kwa maneno, nitafoka kwa kalamu,” alisisitiza.

Rais Samia alikuwa anaanza kuwaonesha watumishi na Watanzania kuwa katika kipindi cha miezi sita ya urais wake alijaribu kuwa mkimya na mtulivu kwa lengo la kuwasoma lakini pia kusoma wizara zote ili kuona mambo ya kurekebisha.

“Wapo pia ambao wakati nawasoma nao walinisoma; wapo waliochukulia ukimya wangu na utulivu wangu kama udhaifu na wengine wakafanya kazi nzuri,” alisema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi aliendelea kuwakumbusha wateule wake kuwa wasidhani kuwa yeye ni mpole kwani upole wake huzungumza kwa kalamu.

“Najua kuna wanaonitazama nilivyo na wakasema huyu mama hamna kitu. Nilisema ndani ya miezi sita nilikuwa nawasoma na ninyi mmenisoma kwa hiyo sasa tumesomana kazi iendelee,” alibainisha.

“Nilisema kwenye mikutano nilipowaapisha mawaziri niliowabadilisha kuwa sitakaa kwenye viriri kufoka; sijaumbwa, sijakuzwa hivyo. Mimi yangu naangalia utendaji wenu, ambaye upo chini namwambia waziri sijaridhika namtoa. Watu ni wengi mno wanasubiri hizo nafasi, naweka wengine watakwenda kujituma na kutumikia wananchi.

“Msitegemee nitakuiteni fulani na fulani njooni hapa; kwa nini hivi na hivi! Hapana… wote ni watu wazima mnayajua mazuri na mabaya, mkifanya mnafanya makusudi nitaongea kwa kalamu narudia tena,” alisema Rais Samia katika mabadiliko ya pili ya baraza lake la mawaziri Januari 8, 2022. Hata hivi karibuni alipokuwa akiwaapisha mawaziri aliowateua katika mabadiliko aliyoyafanya kwa mara ya nne mwaka huu, alisisitiza tena;

“Nawaombeni sana upole si ujinga, upole wakati mwingine ni maarifa, unalifikiria jambo mara mbili mara tatu kabla hujatoa maamuzi kabla hujatoa karipio, nendeni mkawatumikie wananchi.”

MATENDO MAKALI

Yamkini sasa tunaweza kusema upole ndiyo sura ya Rais Samia; matendo yake yanaongea kwa ukali na si kuzungumza kwa ukali.

Wateule wengi sasa wameanza kumwelewa huku wakitekeleza majukumu yao kwa uhuru na ubunifu. Ndiyo maana alipokuwa akizungumza katika kikao cha kazi cha wakuu wa mikoa, Kibaha mkoani Pwani baada ya viongozi mbalimbali kuwanoa, Rais Samia aliendelea kusisitia mojawapo ya faida kubwa ya upole wake kwamba anawapa uhuru watendaji hao kuonesha ubunifu wao.

Uhuru huo una maana kubwa hata katika utendaji wa binadamu yeyote awapo kazini, kwamba kama utakuwa unatekeleza majukumu yako bila kufokewa, utakuwa unajiamini, na ndipo hali ya ubunifu itajitokeza na kufanikiwa kufanya mambo ya msingi ambayo yatakuwa na faida kwako na jamii yako.

Rais Samia alikuwa na maana wakuu hao wa mikoa na viongozi wengine wasisubiri aje awaelekeze nini cha kufanya badala yake waoneshe ubunifu wao.

Pamoja na uhuru huo, kama ilivyo katika Katiba ya Tanzania au sheria kwa ujumla, hakuna uhuru usio na mipaka hii ina maana kuwa kwa viongozi hao nao pia uhuru huo wasiutumie kuwaumiza wengine, kuwaonea wengine badala yake wautumie kuendelea kufikisha kile ambacho serikali imedharimia kukifisha ikiwamo kutatua changamoto zao.

MWAKA WA MABADILIKO 

Katika kuhakikisha wateule wake wanamwelewa, Rais Samia alianza taratibu kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, mbali na nafasi nyingine za juu. Mwaka 2021 alifanya mabadiliko mara moja tu, mwaka 2022 alifanya mabadiliko mara mbili (Januari na Oktoba 2022). Mwaka huu Rais Samia ametumia kalamu kufanya mabadiliko Februari 14, Aprili mosi, Julai 5 na Agosti 30.

Kadhalika katika nafasi nyingine za juu kama vile Mkurugenzi Idara ya Usalama tayari Rais Samia ameweka rekodi ya kubadilisha mara tatu makachero wakuu wa kitengo hicho nyeti. Mabadiliko haya ya mwaka huu yametafsiriwa kuwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2025 pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka kesho.

Rais Samia na wasaidizi wake wamedhihirisha hilo jambo ambalo linazidi kuwaweka mkao wa kuwa tayari kwa majukumu mazito. Kinachosubiriwa na Watanzania ni ubunifu, utekelezaji au uwezo wa wasaidizi wake kutafsiri maono ya kiongozi huyo mkuu wa nchi. Makala hii imeandaliwa na Gabriel Mushi. – 0715126577

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yawaangukia viongozi wa dini

Spread the loveSERIKALI imewaomba viongozi wa dini, waendelee kuelimisha wananchi kudumisha amani...

Habari za Siasa

Azzim Dewji aitaka Serikali iwanyooshe mafisadi

Spread the loveMFANYABIASHARA maarufu nchini, Azzim Dewji, ameitaka Serikali iwachukulie hatua wezi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

error: Content is protected !!