Wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Kongo, Rais Felix Tshisekedi ameendelea kuongoza kwa asilimia 77 na mpinzani wake wa karibu Moise Katumbi akifuatia kwa asilimia 15 katika jumla ya kura milioni tisa zilizohesabiwa hadi sasa.
Hayo yanajiri wakati upinzani ukiendelea kutoa madai ya udaganyifu katika uchaguzi huo na kutaka urudiwe. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Hadi usiku wa kuamkia jana Alhamis, Tume ya Uchaguzi nchini humo (CENI), ilitangaza matokeo ya kura zaidi ya milioni tisa ambazo tayari zimehisabiwa.
Rais Tshisekedi anayewania muhula wa pili ameonekana kupata kura zaidi ya milioni saba ambazo ni sawa na asilimia 77. Mpinzani wake wa karibu Moise Katumbi akiwa na asilimia 15 na Martin Fayulu akishika nafasi ya tatu na silimia 4 pekee.
Tshisekedi anaongoza kwa wingi wa kura katika majimbo 21 kati ya 26 ya Kongo pamoja na jiji kuu la Kinshasa huku Katumbi akiongoza katika majimbo manne ya kusini mashariki yakiwemo Haut-Katanga, Tanganyika, Lualaba na Haut-Lomami.
Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Rais yanatarajiwa kutangazwa jumapili ya tarehe 31 Desemba 2023.
Upinzani umeyapinga matokeo hayo ya awali na kusema yalipangwa na Tume ya uchaguzi ili kumpa ushindi Rais Tshisekedi.
Olivier Kamitatu msemaji wa Moise Katumbi amesema uchaguzi lazima urudiwe na hivi karibuni watawasilisha malalamiko yao kwenye korti ya Katiba.
”Vyombo vyote vinavyosimamia mchakato wa uchaguzi vinaongozwa na wanachama wanaohusishwa na kabila la Félix Tshisekedi. Kwa hivyo, Mahakama ya Kikatiba inaendeleza tu udanganyifu ambao tayari umepangwa,” alisema Kamitatu.
Patrick Muyaya, msemaji wa serikali alikosoa vikali kauli hiyo ya msemaji wa Katumbi na kusema upinzani unapanga kuandaa vurugu.
Muyaya ameiambia DW kwamba machafuko hayatatokea na kuutaka upinzani kusubiri hadi matokeo kamili ya uchaguzi yatakapotolewa.
Leave a comment