January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Familia za Masheikh 186 wanaosota rumande  kwa ugaidi zamuangukia Rais Samia 

Watuhumiwa na kesi ya ugaidi wakifikishwa katika Mahakama ya Kisutu

Spread the love

 

FAMILIA za Masheikh 186 walioko katika  mahabusu ya Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, kwa zaidi ya miaka saba, wakituhumiwa kwa ugaidi, bila kesi zao kusikilizwa kwa madai upelelezi haujakamilika, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie kati ili haki yao ipatikane. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Jumatatu, tarehe 13 Desemba 2021 na wawakilishi wa familia hizo, wakizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Familia hizo zimedai zimeamua kutumia vyombo vya habari kutoa wito huo, baada ya jitihada zao za kuwasiliana na mamlaka husika kutafuta suluhu ya jambo hilo, kugonga mwamba.

Zimedai kuwa, katika nyakati tofauti, zilituma barua zaidi ya sita kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli  na Rais Samia, kwa ajili ya kupeleka maombi yao, lakini hazijajibiwa.

Abdulwahid Hamis Said, ndugu wa Swed Anuary Hatib, ameziomba mamlaka zinazohusika zilifanyie kazi suala hilo, ili haki itendeke.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Tuna ndugu zetu 186  walioko mahabusu Ukonga wako takribani miaka nane hadi tisa,  ndugu yangu anatakribani miaka 9 bado kesi yao haijulikani, mwanzo kwa kuwa tushawaona wamekamatwa lakini tukifuatilia kesi hatujui hatima yake ni nini, hatuambiwi kesi yao inasomwa lini? Tunapouliza tunaambiwa hata miaka 300 itachukua, haitupi picha halisi,” amesema Said na kuongeza:

“Nafahamu Serikali yetu ni sikivu, tunaiomba ione kuwa ina wajibu wa kusimamia sheria zake kama vile inavyotaka na wale wasimamizi wa sheria wawe watu waaminifu, tunaomba ndugu zetu kama hawana hatia waachwe huru na kama ikibainika wana hatia waadhibiwe.”

Zaujia Abdallah, ambaye hajui mahali alipo mume wake  Maulid Said Mbonde, aliyekamatwa tangu June 2017, amemuomba Rais Samia aingilie kati ili ajue hatima ya mume wake aliyemuachia watoto sita huku yeye akiwa hana uwezo wa kuwatunza.

“Sijui mume wangu yuko wapi tangu tarehe 19 June 2017 walivyomchukua katika kazi zake maeneo ya Mwandege. Nimezunguka magereza yote lakini hayupo. Naomba Rais Samia anisaidie maana hapa nilipo ninaumwa ninasumbuliwa na tatizo la mirija ya moyo kusinyaa na sina uwezo wa kufanya kazi kulea watoto sita nilioachiwa, naishi kwa hifadhi na kuomba omba ili mimi na watoto tupate kuishi,” amesema Zaujia.

 

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Zingiwa, Dar es Salaam, Fatuma Nassoro, ameiomba Serikali na chama chake, iwahurumie ndugu zao kwa kuqafikisha mahakamani ili hatma yao ibainike,  kama wana hatia wafungwe na kama hawana hatia waachwe huru.

“Mimi nina kaka yangu Ally Nassoro na Juma Zuberi, wamekamatwa toka 2014 namaanisha mpaka sasa wana miaka nane hadi tisa, toka walipokamatwa wanapelekwa mahakamani, ukienda unaambuwa kesi imeahirushwa upelelezi haujakamilika.Naomba Rais Samia mwenyekiti wangu wa chama unisikilize na kilio hiki ni cha siku nyingi tulinyamaza kimya tukidhani litafanyiwa kzi lakini majibu hatuna. Tunakuomba rais tuone huruma wa mama wenzio,” amesema Fatuma na kuongeza:

“Naomba hawa watu wapelekwe  mahakamani tutaelewa nini shida,  mimi ni katibu wa jumuiya ya wazazi Kata ya Zingiziwa  nimepewa majukumu ya chama nashindwa kuyatekeleza nina watoto watatu  na sita nilioachiwa kiasi kwamba sina uwezo wa kuniendesha, nashindwa kutekeleza majukumu yangu ya kazi ya chama niliyokabidhiwa. Nina imani makatibu wa cham  mtapata taarifa hizi na kuzifanyia kazi.”

 

Aisha Seleman, mke wa Zahak Rashid, aliyeko mahabusu tangu 2018, amemuomba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, afanyie kazi malalamiko yao ili mume wake apate haki yake.

“Tunamuomba mwanamke mwenzetu Mama  Samia sikia kilio chetu pamoja na DPP na Mahakama,  kuchukua jukumu katika hili ambalo ndugu zetu linawakumba,”  amesema Aisha.

Hadija Mohammed Nkondo, mama mzazi wa Idd Seleman Nyange, aliyeko mahabusu tangu alipokamatwa 2015, amemuomba Rais Samia awaonee huruma watoto wao akidai kwamba haki zao zinakiukwa.

Kwa upande wake, Hamid Haruna Mkanda, ambaye ndugu yake aliyeko mahabusu tangu 2015,  ni Abas Ayub Mkanda, ameiomba Serikali isikilize kilio chake kwani kuna baadhi ya wazazi wameoata matatizo ya kiafya kutokana na vijana wao kushikiliwa ndani kwa muda mrefu bila hatima yao kujulikana.

 

“Baba yetu hali yake si nzuri, akimfikiria mwanawe presha inapanda, presha inapanda,  amekopa pesa kumsaidia mwanaye lakini wapi, tangu 2015 mpaka leo juhudi nyingi zimefanyika lakini hazina tija, sisi hatuna uwezo ila tunaiomba Serikali itusaidie,” amesema Mkanda na kuongeza:

“Serikali ilifuatilie suala hili,  ilimalize kwani hakuna linaloshindikana juu ya Serikali. Rais Samia  anaweza kulimaliza, walimalize ili anayestahiki basi achukuliwe hatua. Tunaiomba Serikali sisi ndio wenye ndugu, wako huko tumekwenda sana

kila siku miguu haishi kwenda kuwaangalia hadi uchungu, kibaya zaidi wengine familia zao zimeharibika sana tangu walipokamatwa.”

Mbali na Masheikh hao 186 wanaosota rumande kwa tuhuma za ugaidi, inadaiwa kuna wengine wako katika mahabusu za mikoa mbalimbali, ikiwemo 61 waliomo Arusha, Mwanza (52), Geita (14), Morogoro (21) na Mtwara (25).

Pia, inadaiwa kwamba, kuna kina mama wawili, Mwajumbe Bakari na Kuruthumu Iddy, wako katika mahabusu ya Gereza la Segerea tangu 2014, kwa tuhuma za ugaidi.

error: Content is protected !!