Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi wameshuhudia utiaji saini hati ya makubaliano (MoU) baina ya nchi hizo mbili.
Utiaji saini wa hati hiyo inayohusu ushirikiano katika masuala ya teknolojia (ICT), posta na mawasiliano umefanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam katika ziara siku mbili ya kikazi ya Rais Tshisekedi aliyetua nchini leo.
Mkataba huo unaohusu teknolojia umetiwa saini leo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania, Nape Nnauye pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Mambo ya Nje wa DRC, Christophe Lutundula.
Tanzania na DRC zimekubaliana kushirikiana na kuendeleza sekta ya mawasiliano kwa kuwa ni sekta pekee inayozalisha rasilimali pamoja na ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.
Katika kukuza jitihada za biashara baina ya nchi hizo mbili, Rais Samia Serikali inafanya marekebisho ya meli ya Mv Sangara ili ianze tena kutoa huduma ya kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na DRC.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania na DRC kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki zina mpango wa kujenga ushoroba wa kati wa barabara utakaounganisha nchi hizo mbili.
Takwimu za biashara baina ya nchi hizo mbili zimepungua kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita hivyo nchi hizo mbili zimefufua Tume ya pamoja ya ushirikiano ili kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Leave a comment