MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Tanga, imemuachia kwa masharti Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ahmed Kidege na wenzake wawili, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kuiomba ifute kesi ya ugaidi iliyokuwa inawakabili mahakamani hapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Masharti hayo ni, kuwa katika kipindi cha uangalizi wa muda wa miaka mitatu, ambapo Kidege na wenzake watakuwa wanaripoti Polisi kila Jumatatu ya mwanzo wa mwezi.
Taarifa hiyo imetolewa jana tarehe 25 Februari 2022 na Katibu Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalum, ACT Wazalendo- Taifa, Mbarala Maharagande, muda mfupi baada ya Kidege na wenzake wawili, Ramadhani Songoro na Shaban Mohamed.
“Tarehe 25 Februari, 2022, Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga imefuta kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi, iliyokuwa inamkabili dege na wenzake wawili. Hatua hiyo ya mnahakama imetokana na DPP kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo,” imesema taarifa ya Maharagande.
Kidege na wenzake walikaa rumande tangu tarehe 24 Septemba 2019.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema anaamini hayo masharti ya kuripoti Polisi, aliyopewa Kidege na wenzake, yataondolewa.
“Ni jambo la faraja kwa familia, chama na wapenzi wa haki nchini kuona Kidege na wenzake wameachiwa huru na kesi yao kufutwa baada ya kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka miwili. Kwetu sisi, kila mwenzetu anaposhikwa na kufunguliwa kesi, kitu muhimu zaidi kwetu ni uhuru wake,” amesema Ado na kuongeza:
“Kwa namna yoyote ile. Ni matumaini yetu kuwa kupitia jitihada zetu, hata hayo masharti madogo ya kuripoti Polisi mara moja kwa Mwezi yataondolewa.”
Leave a comment