Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Dk. Mwinyi: Mafanikio miaka 60 ya Mapinduzi yametokana na waasisi, viongozi waliotangulia
Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mwinyi: Mafanikio miaka 60 ya Mapinduzi yametokana na waasisi, viongozi waliotangulia

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi
Spread the love

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Zaraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio waliyoyapata miaka 60 tangu Mapinduzi ya mwaka 1964, yametokana na uongozi thabiti wa waasisi wa Taifa hilo na viongozi wote wa awamu zilizotangulia kwa ushirikiano na uzalendo kati yao na nyinyi wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Amesema Serikali ya Awamu ya Nane tokea ilipoingia madarakani miaka mitatu iliopita, inayaendeleza mafanikio hayo na kufanya juhudi za kuhakikisha Zanzibar inazidi kupiga hatua za maendeleo katika sekta zote na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo jana tarehe 11 Januari katika hotuba yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapindduzi ya Zanzibar.

Amesema alipoingia madarakani mwaka 2020, alieleza dhamira yake ya kuunganisha malengo ya Mapinduzi na uchumi, akilenga kuimarisha jitihada za kukuza uchumi ili kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar.

“Lengo la Serikali ninayoiongoza ni kuendeleza umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika kuifikia dhamira hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane,” amesema.

Amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, wanafurahia kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano.

Uwanja wa ndege Zanzibar.

“Misingi hii muhimu imetuwezesha kupiga hatua katika maendeleo ya uchumi, ujenzi wa miundombinu, kuimarisha huduma za jamii, biashara na kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” amesema.

Amesema juhudi zinazochukuliwa na Serikali yake zimewezesha uchumi Zanzibar kuzidi kuimarika ambapo thamani ya Pato halisi la Taifa (GDP) imeongezeka kutoka Sh. 3.116 trilioni kwa mwaka 2020 na kufikia thamani ya Sh. 3.499 trilioni mwaka 2022.

Vilevile ukusanyaji wa mapato umeongezeka kufikia Sh. 1.4 trilioni mwaka 2022/2023 kutoka Sh. 790.48 bilioni mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asimilia 56.4.

Aidha, amesema kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2022 imefikia wastani wa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020.

Amesema kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea.

Feri Zanzibar

“Kukua kwa uchumi wetu kumetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwa kutekelezwa miradi ya Maendeleo ya kipaumbele ikiwemo miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za maji safi na salama, uimarishaji wa huduma za nishati ya umeme, masoko na kuimarika kwa sekta ya huduma kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii.

“Pato la mtu binafsi nalo limeongezeka kutoka USD 1,099 sawa na Sh 2.5 milioni mwaka 2020 na kufikia USD 1,230 sawa na Sh. 2.8 milioni mwaka 2022.

Amesema sekta ya biashara ya usafirishaji na uingizaji bidhaa kwa ujumla inaendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022 Zanzibar imefanya biashara yenye thamani ya Sh. 1.4 trilioni ukilinganisha na Sh. 913.1 bilioni kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 57.6.

“Kuhusu biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha bidhaa zenye thamani ya Sh. 37.64 bilioni ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya S. 15.03 bilioni zilizosafirishwa mwaka 2020. Kwa upande wa uagiziaji katika kipindi cha mwaka 2022, Zanzibar imeagiza bidhaa zenye thamani ya Sh. 375.80 bilioni kutoka Tanzania Bara ikilinganishwa na uagiziaji wa bidhaa zenye thamani ya Sh. 243.81 bilioni kwa mwaka 2020,” amesema.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Nane imekuja na dhana ya Uchumi wa Buluu unaotilia mkazo matumizi ya rasilimali za bahari na shughuli nyengine za kiuchumi zinazohusiana na bahari.

“Mafanikio yamepatikana katika sekta kuu za uchumi wa buluu ambazo ni utalii, uvuvi na kilimo cha mwani, bandari, mafuta na gesi asilia na biashara inayohusiana na usafiri wa majini.

“Kuhusu utalii, ni sekta iliyopewa mazingatio katika kuleta fedha za kigeni na ajira katika awamu zote za Serikali baada ya Mapinduzi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi.

“Juhudi mbalimbali zimefanywa na viongozi wa awamu zilizopita ili kuongeza michango ya sekta hii katika Pato la Taifa pamoja na upatikanaji wa ajira. Sekta ya utalii imeendelea kupata mafanikio makubwa. Idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 143.6, kutoka watalii 260,644 mwaka 2020 hadi 638,498 mwaka 2023. baada ya UVIKO – 19,” amesema.

Katika sekta ya ujenzi amesema Serikali yake imejenga barabara kuu KM 103.5, barabara za ndani mjini na vijijini KM 275 pamoja na ujenzi wa barabara za mjini KM 100 na madaraja ya juu mawili katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Kwa upande wa usafiri wa anga, amesema mapato ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege yameongezeka kutoka Sh. 11.6 bilioni mwaka 2019/2020 hadi kufikia Sh. 29.3 bilioni mwaka 2022/2023.

Aidha, amesema kuna ongezeko kubwa la abiria wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa kutumia Viwanja vya Ndege kutoka abiria 1,609,235 mwaka 2019 (Kabla ya UVIKO – 19) na 840,599 mwaka 2020 (wakati wa UVIKO – 19) hadi kufikia abiria 1,904,459 mwaka 2023.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!