Thursday , 13 June 2024
Home Kitengo Biashara Dk. Biteko aiagiza TPDC kuandaa mpango wa muda mrefu wa upatikanaji gesi
BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aiagiza TPDC kuandaa mpango wa muda mrefu wa upatikanaji gesi

Spread the love

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia ili muda wote kuwe na hazina ya kutosha ya nishati hiyo inayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na katika magari. Anaripoti Mwandishi Wetun …(endelea).

Dk. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 21 Novemba 2023 wakati wa kikao chake na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na Dk. Biteko kuelekeza matarajio ambayo nchi inayahitaji kutoka TPDC.

“TPDC tujiulize, Je uwezo wetu wa kuzalisha gesi asilia unaweza kujibu mahitaji yetu  ya gesi ? tujiulize hili na tuchukue hatua. Tutambue kuwa mahitaji ya gesi asilia ni makubwa kwa sasa kwani dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta na kwenda kwenye gesi asilia hivyo lazima tujipange, na pia tukumbuke tumesaini makubaliano ya kusafirisha nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na Gesi ya kutosha.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Dk. Biteko pia amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, Dk. Biteko amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya Gesi Asilia lazima yabadilike na wapewe huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.

“Nashukuru mmeanza kufanyia kazi maagizo niliyoyatoa kwa haraka, ikiwemo ya kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya Gesi Asilia, kupeleka kivuko kisiwa cha Songosongo na malipo ya mafao kwa wastaafu wa Knight Support ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya gesi asilia Songosongo ambao hawakulipwa muda mrefu, watu hawa wanahitaji huduma bora,” amesema Dkt. Biteko.

Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue

Aidha, Dk. Biteko ameiagiza TPDC kupita kwenye Halmashauri zote nchini zinazopokea ushuru wa huduma kutokana na shughuli za mafuta na gesi asilia kufanyika kwenye Halmashauri hizo ili TDPC ijihakikishie kwamba, fedha hizo zinaenda pia kwenye vijiji/maeneo ambayo shughuli za uzalishaji wa Gesi Asilia zinafanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame alimweleza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, TPDC inaandaa Mpango Mkakati wa Shirika ambao utaweka mikakati ya Shirika kwa kipindi cha miaka 10 na zaidi ili kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia ya kutosha kwa matumizi ya ndani.

Pia TPDC itawekeza zaidi katika mnyororo wa thamani wa Mafuta na Gesi ili kukuza matumizi ya Gesi Asilia na hivyo kuchochea biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, alieleza mipango ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda kuja Tanzania, Mradi wa Gesi ya Kusindika (LNG) ambapo majadiliano yamekamilika na mikataba ipo kwenye hatua za kuidhinishwa, utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Kisiwa cha Songosongo Magharibi unaotarajiwa kuanza Septemba 2025 na utafutaji mafuta kitalu cha Eyasi Wembere ambapo tafiti zinaendelea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake ambayo yamewapa hamasa ya kufanya kazi na wameahidi kwamba wataenda mbali kiutendaji na watatoa ushirikiano kwa Naibu Waziri Mkuu ili kusukuma mbali zaidi Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wafungwa, mahabusu ruksa kupiga kura

Spread the loveTUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kuwa wafungwa,...

Habari za SiasaKimataifa

IFP wakubali kuungana na ANC kuunda serikali

Spread the loveChama cha upinzani nchini Afrika Kusini, Inkatha Freedom Party (IFP)...

BiasharaHabari za Siasa

Prof. Mkumbo: Pato la taifa limefikia trilioni 148

Spread the loveWaziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mwaka...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Deni la Serikali lafikia trilioni 91

Spread the loveWaziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema hadi...

error: Content is protected !!