ILI kutimiza malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwajengea uwezo na kuwainua wakandarasi wa ndani, katika mwaka wa fedha 2023/204, jumla ya miradi minne ya barabara yenye urefu wa kilometa 200 imetengwa kwa ajili ya kuwapa zabuni wakandarasi wazawa.
Pia jumla ya kilometa 20 za barabara zimetengwa kwa ajili ya wakandarasi wanawake, ambapo zitagawanywa katika vipande vya kilometa tano tano, na kazi hizo zitashindanishwa kwa makampuni ya wanawake peke yao, hii inafanya jumla ya km 220 kujengwa na wakandarasi wazawa kwa mwaka 2023/24. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo tarehe 21 Novemba, 2023 katika Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na wakandarasi wazawa na washauri elekezi wa ndani jijijini Dodoma, kujadili nafasi yao katika utekelezaji wa miradi.
Bashungwa amesema wizara ya ujenzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kutenga miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa ajili ya wakandarasi wa ndani kwa lengo la kuwasaidia kukua na kupata uzoefu.
“Katika mwaka wa fedha 2023/204, jumla ya miradi minne ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 kila moja zimetengwa kwa ajili ya wakandarasi wa ndani tu, kwa hiyo kilometa 200 zitajengwa na wazawa, hii ni fursa kubwa ya kuwasaidia wakadarasi”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa kazi za matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zenye thamani ya Sh 600 bilioni zitatekelezwa na wakandarasi wa ndani katika mikoa yote 26 nchini.
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024 kazi zote za matengenezo ya barabara kwa mikoa yote 26 nchini, Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutekelezwa na wakadarasi wa ndani”, amesema Bashungwa.
Pia, Bashungwa amefafanua kuwa sheria ya ununuzi wa umma imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mradi ambao utatekelezwa na wakandarasi wa ndani tu, bila kushindanishwa na Makandarasi wa nje.
Lengo kuu ya mkutano huu ni kujadili na kudadavua mikakati mbalimbali kati ya Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi kuhusu kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na washauri elekezi.
Leave a comment