Viongozi wa vijiji wametahadharishwa kuacha kushirikiana na mafundi vishoka wa umeme kupitia mgongo wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutapeli wananchi fedha huku wakiwaahidi kuwafikishia umeme kwenye nyumba zao. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea)
Wito huo umetolewa leo taerehe 10 Novemba 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Farida Mgomi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Kasanga Kata ya Lubanda.

Ni baada ya kuibuka kwa ajenda ya mkandarasi kuwalipisha fedha wananchi huku zaidi ya wananchi 80 ambao mpaka sasa hawajaingiziwa umeme.
Aidha, Mgomi amewaonya viongozi wa vijiji kuitisha mikutano ya kuhamasisha wananchi kuchangisha fedha za kuingiziwa umeme kupitia REA bila kuwasiliana na Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Ileje.
Mgomi amesema wananchi huchangishwa fedha na mafundi wa umeme maarufu (vishoka) na kuwataka kutoa taarifa pindi wanapowaona ili wakamatwe.
Kwa upande mwingine Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wilayani hapa, Kassian Kipanga amewasihi viongozi wa vijiji waache kushirikiana na mafundi vishoka kuitisha mikutano ya kuhamasisha wananchi kuchangisha fedha za kuingiziwa umeme kwa gharama ambazo hazitambuliki na Serikali.
Naye Mratibu wa nNshati Vijijini (REA) Wilaya ya Ileje Jacob Lugome amesema gharama ya kuingiza umeme vijijini kupitia REA ni Sh 27,000 kwa mkondo wa njia moja na Sh 139,000 kwa mkondo wa njia tatu.
Akielezea madhila wanayotendewa na vishoka hao, mmoja wa wananchi katika Kijiji cha Kasanga, Davison Kasekwa amesema walitozwa fedha hizo mwaka 2017.
Amesema kila mwananchi alitozwa Sh 40,000 lakini mpaka sasa hawajaingiziwa umeme hivyo wanaiomba Serikali kumfuatilia fundi huyo ili achukuliwe hatua za kisheria.
Leave a comment