Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema katika utekelezaji wa Dira ya 2030 yenye kueleza kuwa, “Madini ni Maisha na Utajiri, Tume imejipanga kuboresha usimamizi wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuendelea kutenga maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kijiolojia kwa wachimbaji wadogo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Lengo ni kuwezesha shughuli za wachimbaji wadogo kuwa na tija pamoja na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini nchini.
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo tarehe 10 Novemba 2023 kwenye kipindi cha Goodmorning kilichorushwa mubashara na kituo cha Televisheni cha Wasafi chenye lengo la kuelezea mikakati ya Taasisi za Wizara ya Madini kwenye utekelezaji wa Dira ya 2030 yenye lengo la kuimarisha Sekta ya Madini.
Amesema utekelezaji wa dira hii katika sekta ya madini inawalenga zaidi wachimbaji wadogo wa madini ambao wamekuwa wakiwekeza lakini manufaa yamekuwa si ya kuridhisha kutokana na kutokuwa na taarifa za kutosha za utafiti za madini na teknolojia duni kwenye uchimbaji wa madini.
Amefafanua kuwa Tume itaendelea kuimarisha usimamizi katika shughuli za madini kwa kutenga maeneo yenye taarifa za kijiolojia yaliyofanyiwa tafiti ili kuweza kunufaika na rasilimali hizo.
Pia tume inalenga kuandaa mpango Kazi utakaosimamia maeneo ya elimu za ugani; kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni; ukaguzi migodi na mazingira; usimamizi wa masuala ya afya na usalama mahala pa kazi pamoja na kuimarisha mifumo ya makusanyo ya maduhuli.
Akielezea mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini kwenye utekelezaji wa Dira ya 2030, hususan kwenye ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini Mhandisi Samamba amefafanua kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wamiliki wote wa migodi kuhusu kutoa kipaumbele kwa huduma na bidhaa zote zinazotolewa na watanzania.
Pia tume imepanga kuandaa namna bora ya kuingia ubia kati ya kampuni za watanzania na kampuni za nje na uwepo wa utekelezaji wa sheria ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini pamoja na urejeshaji wa Huduma kwa Jamii.
Leave a comment