Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yamjia juu Spika Tulia kisa mkataba wa bandari
Habari za Siasa

Chadema yamjia juu Spika Tulia kisa mkataba wa bandari

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepinga uamuzi wa Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuzuia wabunge kujadili bungeni sakata la mkataba wa uwekezaji bandarini, kikidai kuwa unalenga kuzuia maoni ya wananchi kufanyiwa kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Simiyu…(endelea).

Mkataba huo uliofungwa kati ya Serikali ya Tanzania na Imarati ya Dubai, juu ya ushirikiano wa uwekezaji bandarini, uliridhiwa na Bunge kwa ajili ya utekelezwaji, tarehe 10 Juni 2023, bungeni jijini Dodoma.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, leo tarehe 29 Agosti 2023, mkoani Simiyu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, amesema wabunge hawakupaswa kupigwa marufuku kujadili mkataba huo, akidai walipitisha azimio la kuuridhia bila kuusoma na kujua kilichomo ndani yake.

“Leo Spika wa Bunge amewapiga marufuku wabunge kujadili suala la bandari za nchi hii kukabidhiwa kwa waarabu wa Dubai, walipopitisha huu mkataba walipewa siku mbili na mimi nafahamu jinsi Bunge letu linavyofanya kazi, nafahamu kwamba hakuna mbunge hata mmoja aliyeusoma ule mkataba na kuuelewa,” amesema Lissu.

Lissu ameenda mbali zaidi kwa kudai kuwa, hata Rais Samia alitoa idhini kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, asaini mkataba huo kwa niaba yake, bila kujua kilichomo ndani yake.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Susan Kiwanga, amesema “nataka kupeleka salamu kwa Spika wa Bunge, amesikika leo bungeni akisema kwamba kuna mkataba na azimio walipitisha bungeni la mkataba wa bandari zetu za Tanganyika. Wananchi wanajadili hawakubaliani na vifungu vilivyopo kwenye mkataba wa Dp World,”

“Walioko bungeni ni wawakilishi wetu wananchi, wamesikia kelele zetu lakini wanatoa jibu huo mkataba umeshapita sisi wananchi tungoje mikataba mingine itakayokuja, wewe Spika Tulia shika huwezi ukalishawishi Bunge na huo mkataba haukubaliki ufutwe mara moja,” amesema Kiwanga.

Mapema leo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliwataka wabunge kutotumia vikao vya mhimili huo vinavyoendelea kutoa ufafanuzi wa kujibu hoja za wananchi kuhusu mkataba wa uwekezaji bandarini, hadi pale kutakapokuwa na ulazima wa kuzungumzia suala hilo.

“Hatutatumia Bunge hili kutoa ufafanuzi ama kujibu hoja za wananchi, ni kazi yetu kuzipokea hoja hizo na pale tunapoona uko ulazima basi Bunge litaleta hoja hizo mezani na tutaweza kuzijadili kwa pamoja na kufanya maamuzi kama Bunge,” amesema Spika Tulia.

Spika Tulia alisema, wabunge hawapaswi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa Bunge limeshafanya maamuzi dhidi yake, hivyo waendelee kukusanya maoni ya wananchi juu ya uwekezaji wa bandari kwa ajili ya kuyafanyia kazi katika mikataba mingine ya utekelezaji wa miradi, itakayokuja baadae.

“Wakati wetu wa kuzungumza tena juu ya jambo hili sababu tulishafanya maamuzi, ni pale ambapo sheria inatupa nafasi nyingine wabunge tukitaka serikali ilete mikataba hapa bungeni kuijadili, hoja itakuwa mbele yetu na kwa hivyo mawazo tunayoendelea kuyasikia kutoka kwa wananchi wakati huo  tutaweza kuiambia Serikali nini inapaswa kufanya,” amesema Spika Tulia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

error: Content is protected !!