May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema: Serikali itoe taarifa sahihi za corona, chanjo

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali ya Tanzania, kupima na kutoa takwimu za maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Kwamba, kufanya hivyo kuwawezesha wananchi na Jumuiya za Kimataifa, kutambua hali halisi ya maambukizi ilivyo nchini.

Pia, chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimeitaka serikali kuruhusu chanjo ya kujikinga na maambukizi ya corona, kama ilivyo kwa mataifa mengine ulimwenguni ikiwemo Afrika Mashariki.

Hayo yamelezwa leo Ijumaa tarehe 5 Machi 2021, na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipozungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

“Mara ya mwisho Serikali ya Tanzania kutoa takwimu za upimaji wa corona ilikuwa Aprili 2020, toka wakati huo mpaka sasa, serikali haijawahi kutoa takwiku zozote, iwe kiwango cha vifo au maambukizi,” amesema Mnyika.

Amesema, Shirika la Afya Duniani (WHO), limeilalamikia Serikali ya Tanzania kwa kutotoa taarifa sahihi za maambukizi ya corona, hivyo “Chadema tunaitaka serikali iweze kutekeleza kwa haraka zoezi la upimaji na utoaji wa takwimu.”

Kuhusu chanjo, Mnyika amesema, mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Afrika Mashariki (Rwanda na Kenya), tayari yamepokea chanjo ya kujikinga na maambukizi lakini “sisi Tanzania hatuoneshi utayari katika hili.”

Kiongozi huyo amesema, hatua ya Tanzania kutokubali chanjo, kunawafanya mahujaji wanaotaka kwenda kuhiji Makha nchini Saudi Arabia kukosa fursa hiyo.

Amesema, zaidi ya mwezi mmoja umepita tangu Rais John Magufuli alipozungumzia suala la chanjo, na kuitaka Wizara ya Afya kuwa makini na chanjo hizo.

“..na sasa ni wakati wa kuambiwa, nini kinaendelea baada ya agizo hilo sasa. Jitihada zinaendelea mpaka sasa za kuwafanya Watanzania kukataa chanjo.

“Saudi Arabia imesema, watu ambao hawajachanjwa hawatokwenda kuhiji. Tunaitaka serikali iruhusu chanjo ili wanaotaka kwenda kuhiji, wapate hii fursa,” amesema Mnyika.

Mtendaji mkuu huyo wa Chadema ametumia fursa hiyo kutoa wito kwamba “Chadema tunarudia kutoa wito kwa Watanzania kufanya jitihada za kujikinga ikiwemo kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka.”

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

Tarehe 27 Januari 2021, akizindua shamba la miti la Silayo wilayani Chato, mkoani Geita Rais Magufuli alisema, hana mpango wa kuifunga nchi (lock down), kutokana na hofu ya corona, huku akiwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari akisisiza wasitishwe.

“Katika kipindi hiki, magonjwa yanayojitokezatokeza yasiyojulikana kama corona, nchi nyingi wananchi wake watakuwa wamejifungia ndani. Sisi Watanzania hatujajifungia ndani na hatutegemei kujifungia ndani,” alisema.

Kuhusu chanjo Rais Magufuli alisema, kama wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo, basi chanzo za magonjwa mengine kama kansa, kifua kikuu na malaria wangekuwa wameishazipata.

“Chanjo hazifai, kama wazungu wangekuwa wana uwezo wa kuleta chanzo, hata chanjo ya UKIWMI ingekuwa imeishaletwa, hata chanjo ya kifua kikuu… kifua kikuu kingekuwa kimeisha ondoka, hata chanzo ya maleria ingekuwa imesihapatikana, hata chanjo ya kansa ingekuwa imeishapatikana,” amesema.

Amewataka Watanzania kuwa waangalifu kwa kile alichoitwa ‘mambo ya kuletewa letewa,” na kwamba, Watanzania wasifikirie wanapendwa sana na mataifa ya nje.

“Na niiombe Wizara ya Afya isiwe inakimbilia machanjo chanjo bila yenyewe kujiridhisha. Ipo nchi fulani walichanjwa watoto wake wa kike wenye umri wa miaka 14, wanaambiwa ni kwa ajili ya kuzuia kansa ya kizazi, imekuja kugundulika ile chanjo ni ya kuwazuia wasizae.

“Niwaombe sana Wizara ya Afya, sio kila chanjo ni ya maana sana kwa taifa letu, sio kila chanjo ina faida kwetu, ni lazima Watanzania tuwe macho. Ni lazima Watanzania tuwe waangalifu. tutafanyiwa majaribio ya ajabu ambayo yataleta madhara makubwa,” alitahadharisha.

error: Content is protected !!