Sunday , 25 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema kumzika Tambwe Hiza kwa heshima kubwa
Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumzika Tambwe Hiza kwa heshima kubwa

Spread the love

DAKTARI Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), amesema chama hicho kitamzika kwa heshima kubwa, Richard Tamwilay Hiza, mwanachama wake mashuhuri aliyefariki dunia jana. Anaripoti Charles William … (endelea).

Richard Hiza, maarufu kwa jina la Tambwe alifariki dunia usiku wa kuamkia jana, kutokana na ugonjwa wa pumu, ikiwa ni siku moja tu tangu apande jukwaani kumnadi Salum Mwalimu, mgombea katika jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chadema.

“Alikuwa mwanasiasa wa aina yake, mahiri kwa kuzungumza jukwaani, akitumia lugha nyepesi kueleweka na wananchi anapojadili mambo mbalimbali ya kitaifa, sisi kama chama hili ni pigo kubwa sana kwetu,” ameeleza Dk. Mashinji.

Mashinji aliwasili eneo la msiba, nyumbani kwa marehemu Mbagala Kizuiani saa nane mchana wa leo akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa Chadema akiwemo Henry Kilewo, Reginald Munisy na John Mrema.

Amesema, wiki mbili zilizopita alifanya mazungumzo na Tambwe kuhusu mikakati ya uenezi wa Chadema katika sehemu mbalimbali za nchi na walikubaliana kuanza utekelezaji wa mipango hiyo baada ya kumalizika kwa chaguzi ndogo zinazoendelea.

“Aliniambia Katibu Mkuu, subiri tumalize kampeni, halafu nitakuja nianze kazi hiyo, lakini ndiyo hivyo Mungu amemchukua. Tambwe alikuwa mtu wa watu, hata baada ya kifo chake wengi walikuwa hawajui yeye ni dini gani kwasababu alikuwa mtu wa kujichanganya na watu wote.

“Kampeni za Chadema zimesimama mpaka pale tutakapompumzisha mpiganaji wetu,” amesema Dk. Mashinji.

Charles Hiza, mdogo wa marehemu amesema familia hiyo itamkumbuka daima Tambwe kutokana na upendo na urafiki wake na wanafamilia wote ikiwemo ucheshi.

“Hata kama kulikuwa na ugomvi katika familia, Tambwe alikuwa ni mtu anayeweza kuupoza kwa kufanya utani na mambo yakakaa vyema, hakika alikuwa ni kipenzi chetu, tutamkumbuka daima,” ameeleza.

Msemaji huyu wa familia, amesema Tambwe atazikwa katika makaburi ya Chang’ombe Jumamosi, (10 Februari, 2018), ambapo mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa hospitaliti ya Temeke utapelekwa nyumbani kwake Mbagala Kizuiani ili kuagwa kuanzia saa tatu kamili asubuhi mpaka saa saba mchana, kabla ya kuelekea makaburini.

Mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa ni miongoni mwa watu mashuhuri waliofika nyumbani kwa marehemu ili kutoa pole kwa familia yake siku ya jana. Salum Mwalimu, Mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Kinondoni naye alifika msibani hapo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Biteko afuta likizo watumishi Tanesco, bosi Morogoro yamkuta

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk. Doto...

Habari za Siasa

Mbarala ajitosa kumrithi Zitto, aahidi kuipa ushindi ACT-Wazalendo uchaguzi mkuu

Spread the loveKATIBU wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalum...

error: Content is protected !!