December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bibi wa miaka 85, ahofiwa kudhulumiwa ardhi yake 

Spread the love

BIBI wa miaka 85 Tumu Haji Mbonde, anahofia kuporwa ardhi yake ya hekari tano iliyoko kijiji cha Mgomba Kaskazini, wilayani Ikwiriri mkoa wa Pwani na Salehe Said Mtonga. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, hivi karibuni Tumu amedai Mtonga amekuwa akitumia baadhi ya Polisi kuisumbua familia yake, akimshinikiza aondoke katika ardhi aliyojenga makazi yake tangu 2005.

Kufuatia sakata hilo, Tumu ameiomba Serikali iingilie kati ili haki itendeke, akidai Mtunga amekuwa akimsumbua aondoke bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kufungua kesi mahakamani.

“Mtunga ananisumbua, hapa nimekaa zaidi ya miaka 15, lakini anakuja anasema eneo ni la kwake. Kuna wakati alikuja kunisumbua lakini aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji ambaye kwa sasa amefariki dunia alinipatia hati ya kijiji inayonitambulisha kwamba mimi ni mmiliki,” amedai Tumu.

Bibi huyo mwenye watoto wanane amedai “licha ya mimi kupewa hati hiyo, bado Mtunga anaendelea kunisumbua, ananiletea polisi wanakuja kukamata watoto wangu nyumbani. Ameenda kwenye Baraza la Kata la Ardhi, kanifungulia shauri lakini limetolewa uamuzi bila ya mimi kusikilizwa. Matokeo yake anakuja na hukumu ambayo mimi sijapatiwa, akitaka niondoke.”

Mtandao huu ulimtafuta Mtonga kwa njia ya simu, ili kupata ukweli juu ya madai hayo, ambaye hakupatikana kwa zaidi ya wiki mbili na alipoandikiwa ujumbe mfupi napo hakujibu.

Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgomba Kaskazini, Shaban Mbelai amedai ardhi hiyo ilikuwa mali ya Mtunga, na kwamba alimkaribisha Tumu kwa ajili ya kujenga makazi aishi na familia yake.

“Hilo suala limekwisha malizika, limefikishwa mahakamani, katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji mwanzoni mwa 2022, wao wakatengua wakaambiwa pale walipokaa sio mahali pao waondoke na nakala walipatiwa na Mtonga,” amedai Mbelai.

Mbelai amedai kuwa, Tumu amekuwa akiitwa mara kadhaa katika vyombo vya kisheria kwa ajili ya kusikiliza mashauri yanayofunguliwa na Mtunga, lakini hakuhudhuria, kitendo kilichopeleka vyombo hivyo kutoa maamuzi bila ya ushiriki wake.

“Hilo suala limekwisha malizika, limefikishwa mahakamani, katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji mwanzoni mwa 2022, wao wakatengua wakaambiwa pale walipokaa sio mahali pao waondoke na nakala walipatiwa na Mtunga.”

“Huyo mama na Mtonga walikuwa kama mtu na rafiki yake, walikuwa maeneo ya bondeni, baada ya sisi kutoa maeneo walime kwa ajili ya kilimo cha mihogo, Mtonga alikuja Serikali ya Kijiji akahitaji eneo, wakalima. Siyo yeye (Tumu) alipewa, walipewa wananchi wote walime lakini waziwekeze,” amedai Mwenyekiti huyo na kuongeza:

“Eneo alipewa Mtonga, halafu yeye akampa mwenzie. Mfano wewe una mume  amepata eneo maana yake mumeo ni mshirika wako, akaja kumwambia kule kuna eneo tukalime wakakusanyika wakaja pamoja na yeye Mtonga anavyodai eneo ni lake alimkatia kipande Tumu.”

Kufuatia maelezo hayo, MwanaHALISI Online, irudi tena kwa Tumu kwa ajili ya kupata maelezo zaidi, ambaye alidai maelezo ya Mbelai si ya kweli, kwa kuwa na yeye alipatiwa shamba kupitia mchakato huo.

Bibi huyo amedai kuwa, Mtonga hakupeleka kesi mahakamani na badala yake aliipeleka Baraza la Ardhi la Kata, bila ya kushirikishwa.

error: Content is protected !!