BEI ya mafuta ya petroli kwa mwezi Oktoba 2023, imepanda kwa Sh. 68, huku dizeli ikiongezeka kwa Sh. 189. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Mabadiliko hayo yametolewa jana tarehe 3 Oktoba 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),Dk. James Mwainyekule.
Taarifa ya Dk. Mwainyekule, imetaja sababu za ongezeko hilo ni kupanda kwa gharama zake katika soko la dunia, uamuzi wa wazalishaji wakubwa duniani (OPEC), kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo Urusi imewekewa na mataifa ya magharibi.
Bei ya mafuta ya petroli katika Mkoa wa Dar es Salaam, imeongezeka kutoka Sh.3,213 iliyokuwepo Septemba 2023, hadi kufikia Sh. 3,281 itakayotumika Oktoba mwaka huu. Kwa upande wa Dizeli, katika mkoa huo bei imepanda kutoka Sh. 3,259 (Septemba), hadi kufikia 3,448 (Oktoba).
Kwa upande wa Tanga, bei ya Petroli imeongezeka kutoka Sh. 3,259 (Septemba) hadi kufikia 3,327 (Oktoba). Mafuta ya Dizeli yamepanda kutoka Sh. 3,305 (Septemba) hadi Sh. 3,494 (Oktoba).
Bei ya mafuta ya Petroli Mtwara imepanda kutoka Sh. 3,285 (Septemba), hadi kufikia Sh. 3,353 (Oktoba).
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo (Price cap) au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price), kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2023,zilizotangazwa kupitia 2 Gazeti la Serikali Na. 421 la tarehe 23 Juni 2023,” imesema taarifa hiyo.
Leave a comment