July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Algeria yatangaza rais wa mpito

Abdelkader Bensalah

Spread the love

BUNGE la Algeria limemtangaza rasmi Abdelkader Bensalah kurithi mikoba ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Chombo hicho cha kutunga sheria nchini Algeria kimetanga uamuzi huo tarehe 9 Aprili 2019,  moja kwa moja katika kituo cha televisheni ya taifa .

Bunge hilo limebainisha kwamba, Bensalah atakuwa kiongozi wa mpito hadi pale taifa hilo litakapo fanya uchaguzi wake wa urais hivi karibuni.

Bunge hilo limemtangaza Bensalah kuwa rais wa mpito, baada ya halmashauri ya kikatiba Algeria wiki iliyopita kutangaza nafasi ya urais nchini humo kuwa wazi, kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa Bouteflika hivi karibuni.

Hata hivyo, wapinzani nchini humo wamepinga Bensalah atakaye kuwa rais wa Algeria katika kipindi cha siku tisini mfululizo, kushikilia wadhifa huo wakidai kwamba alikuwa ni mshirika mkuu wa Rais aliyejiuzulu, Bouteflika.

Mnamo Aprili 2, 2019, Bouteflika aliyedumu madarakani kwa zaidi ya miaka 20 alitangaza uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wa urais, kufuatia shinikizo la raia wa nchi hiyo na Jeshi, lililotaka ajiuzulu kutokana na kiongozi huyo kupoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi kufuatia kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi.

Kabla ya kushinikizwa kujiuzulu, Bouteflika  alitangaza nia ya kugombea tena kiti cha urais wa Algeria katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

error: Content is protected !!