September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ajali ya bodaboda, mwendokasi yauwa wawili Dar

Spread the love

 

WATU wawili wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la mwendokasi na pikipiki ‘bodaboda’, kwenye barabara ya mwendokasi, maeneo ya Lumumba jijini Dar es Salaam. Anaripoti Noela Shila…(endelea).

Taarifa ya ajali hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 9 Septemba 2021 na Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro, akizungumza na wanahabari jijini humo.

Kamanda Muliro amesema ajali hiyo imetokea jana usiku, kwenye taa za kuongozea magari, baada ya pikipiki kugongana na basi la mwendokasi.

“Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 21:20 usiku, katika barabara ya mwendokasi eneo la Lumumba, kwenye taa za kuongozea magari. Ambapo pikipiki yenye namba za usajili MC 663 CDX, aina ya Boxer ikiendeshwa na Sami Riyaz Khan(17),Mkazi wa Gerezani,”

“Akiwa na abiria wake Patrick Chohan (16), iligongana na basi la mwendokasi lenye namba za usaji T 880 DGV, aina ya Golden Dragon, lililokuwa likitokea Kimara kuelekea Kivukoni na kusababisha vifo vya dereva wa pikipiki na abiria,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema, uchunguzi wa awali unaonyeha chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa pikipiki kujaribu kupita katika taa nyekundu kinyume cha sheria.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, chanzo cha ajali ni dereva wa pikipiki kujaribu kupita taa nyekundu kinyume cha sheria, ndipo walipogongwa na gari la Mwendokasi na kufariki dunia wote,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amewataka madereva wa pikipiki kutii sheria za usalama barabarani, hasa taa za kuongezea magari, kuvaa kofia ngumu na kutopita kwenye barabara za mwendokasi.

error: Content is protected !!