WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kutimiza wajibu kwa kufuata sheria za usalama barabarani kukabiliana na ajali za mara kwa mara ikiwamo katika barabara za mwendokasi Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu….(endelea)
Majaliwa ametoa wito huo leo tarehe 9 Septemba jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba (CCM)
Tarimba alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti madereva wa mabasi ya mwendokasi na pikipiki wanaovunja sheria za usalama barabara kwa kuendesha kwa kasi na kusababisha ajali.
Tarimba alitolea mfano ajali iliyotokea jana katika barabara ya mwendokasi na kusababisha vifo vya watu watatu waliokuwa kwenye pikipiki.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amekiri kuwa ni kweli madereva pikipiki maarufu kama bodaboda wamekuwa hawazingatii sheria ya usalama barabarani.
Amesema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kimekuwa kinatoa elimu ya matumizi ya sheria barabarani kupitia televisheni mbalimbali nchini.
“Nitoe wito kwa Watanzania kuwa ni muhimu kuzingatia sheria za barabara kulinda uhai wa watumiaji wote.
“Kuhusu njia za mwendokasi tumetenga kwa ajili ya magari ya mwendo kasi hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kutekeleza sheria na kujali matumizi ya barabara hizi,” amesema.
Leave a comment