ALIYEKUWA Mkuu waWilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, wamesomewa upya mashtaka matano katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 27/2021, inayowakabili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo…(endelea).
Sabaya na wenzake walisomewa mashtaka hayo, leo Alhamisi, tarehe 9 Septemba 2021 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas, mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda.
Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine ni, John Aweyo, Watson Mwahomange, Enock Mnkeni, Sylvester Nyegu, Nathan Msuya na Jackson Macha.
Wakili Gervas aliwasomewa washtakiwa mashtaka hayo, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuipa mamlaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu, chini ya kifungu cha 12 (3), cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Sabaya na wenzake walisomewa mashtaka hayo ikiwemo, kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuchukua rushwa Sh. 90 milioni, kutoka kwa Francis Mrosso.
Na shtaka la kumtishia Mrosso kumfunguliwa mashtaka ya kukwepa kodi, kinyume cha sheria kwa lengo la kujipatia kiasi tajwa cha fedha.
Lingine ni matumizi mabaya ya madaraka akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, linalomkabili Sabaya peke yake, pamoja na shtaka la kujihusisha na kitendo cha rushwa na kuongoza genge la uhalifu yanayowakabili wote.
Sabaya na wenzake, waliyakana mashtaka hayo baada ya kusomewa, kisha Hakimu Kisinda aliiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 13 Oktoba 2021, ambapo imepangwa kuwa siku ya hoja za awali za kesi kusomwa.
Leave a comment