Monday , 13 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge wacharuka bungeni sakata la umeme
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge wacharuka bungeni sakata la umeme

Spread the love

SAKATA la uhaba wa umeme limeteka mjadala wa taarifa ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa 2023, baada ya wabunge kupaza sauti zao wakiitaka Serikali kuchukua hatua za kutafuta mwarobaini wake,  huku baadhi yao wakiitaka iwashirikishe wawekezaji wa sekta binafsi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mjadala huo umeibuka leo tarehe 6 Februari 2024, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo, kuwasilisha taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Shaban Ng’enda, ameishauri Serikali ikaribishe sekta binafsi katika kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji umeme kwa kuwa ina gharama kubwa ndio maana kuna upungufu wa nishati hiyo.

“Kuhusu suala la umeme, gharama ya uzalishaji umeme ni kubwa sana na hasa miundombinu ya uzalishaji. Leo tunakwenda kukamilisha bwawa lililojengwa kwa zaidi ya Sh. 6 trilioni zimetumika ikiwa karibu ya asilimia 18 ya bajeti nzima ya nchi,” amesema Ng’enda na kuongeza:

“Ninachokusudia kusema Serikali isijibebeshe mzigo mkubwa wa kuendelea kuanzisha miradi, ikaribishe sekta binafsi ili iweke mifumo kuhakikisha wanazalisha umeme kwa njia ya ubia au mikabata, wazalishe kisha TANESCO ununue na kuwapa huduma wananchi.”

Kwa upande wake Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Musukuma), ameishauri “TANESCO kufanyiwe maboresho na muwekeze kwenye ile miradi ya mifano. Vile vituo muwape sekta binafsi wafanye biashara, sekta binafsi zimeunfwa kwa ajili ya biashara nyie hamtaweza.”

Mbunge Viti Maalum, Ridhiki Lurida, amedai tatizo la uhaba wa umeme linasababishwa na baadhi ya watu wanaohujumu miradi ya uzalishaji umeme kwa maslahi yao binafsi na kuitaka Serikali kuwachukulia hatua.

Amedai kuna baadhi ya watu wanafanya njama za kuukwamisha mradi wa kujenga bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere, liliko wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, ili nishati hiyo isizalishwe kwa ajili ya kupata fursa ya kufanya biashara za kuuza majenera.

“Kuna watu wanachepusha maji hali hii siyo ya kuiachia, nimetembea kutoka Lindi mpaka Dar es Salaam, Daraja la Mkapa katika bonde kuna tuta la mchanga hakuna maji yanayokwenda Mafia, hii athari ni kubwa watu wanacheza na mifumo ya maji Bwawa la Mwalimu Nyerere halitafanya kazi itakuwa historia na kuna watu wameapa halitofanya kazi,” amesema Lurida.

Sakata la umeme limekuwa pasua kichwa tangu mwishoni mwa 2023, ambapo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, aliagiza hatua madhubuti zichukuliwe ili kuondoa athari zake hususan mgawo wa umeme.

2 Comments

  • Duh! Jenereta zinaharibu mazingira na kuchafua hewa. Wananchi susieni jenereta….waonje. joto la jiwe!
    Ni aibu kushindwa kumaliza Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kwa wakati. Inaashiria rushwa au mikakati ya kuitumia kisiasa kuliko kiuchumi.
    Siasa bila mafanikio ya kiuchumi ni ulemavu wa fikra.

  • Wabunge mmeshindwa kumsaidia Mama Samia kwa kuhakikisha mradi wa Bwawa la Julius Nyerere umekamilika kwa wakati. Kama wakorea na wajapani wanakamilisha miradi kwa wakati, ni wazi wamisri imewashinda.
    Inasikitisha!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?

Spread the loveDayosisi 7 za KKKT katika kanda ya Ziwa na Magharibi,...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Dk. Biteko: Serikali itaendelea kushirikiana na Red Cross

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Dk.Mpango aagiza trafki kuvaa makoti ya kamera kudhibiti rushwa

Spread the loveMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk....

Habari za SiasaKimataifa

Palestina mwanachama wa 194 wa UN

Spread the loveBaraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa limepitisha kwa...

error: Content is protected !!