Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mgomo Kariakoo ngoma nzito, wafanyabiashara wamtaka Rais Samia
Habari Mchanganyiko

Mgomo Kariakoo ngoma nzito, wafanyabiashara wamtaka Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

MGOGORO wa kodi katika Soko la Kimataifa la Kariakoo umechukua sura mpya baada ya baadhi ya wafanyabiashara kutishia kuendelea kufunga maduka yao hadi watakapokutana na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamejiri leo Jumatatu, jijini Dar es Salaam, baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, kuwataka wafungue maduka hayo ili kupisha mazungumzo kati yao na Serikali, kwa ajili ya kutafuta suluhu.

Makalla alifika sokoni hapo mapema leo, baada ya wafanyabiashara hao kutishia kufunga maduka kwa muda usiojulikana, hadi pale malalamiko yao ya kikodi yatakapofanyiwa kazi.

Makalla aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), isitishe operesheni zake sokoni hapo kwa muda hadi ufumbuzi wa mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi.

Pia aliagiza uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, kuunda timu itakayokwenda kuzungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tarehe 18 Mei 2023, jijini Dodoma.

Licha ya maagizo hayo wafanyabiashara wengi walionesha kutoridhishwa nayo wakidai hayatafanyiwa kazi kwa kuwa sio mara ya kwanza kutolewa.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Ghalib Suleiman, amesema kama malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo hayatatatuliwa, mgomo huo utasambaa nchi nzima.

Baadhi ya maduka ya Kariakoo yakiwa yamefungwa

“Kariakoo ndio Tanzania na kitovu cha Biashara nchini, jambo lolote linaanza kwa wakubwa, nyie mnawapa machaguzi wenzenu mkisema kufunga maduka nchi nzima wafanyabiashara wako tayari hata kuhamia Dodoma kwa ajili ya kuzungumza na Rais,” amesema Suleiman.

Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Peter Mbilinyi, amesema wamemua kuchukua uamuzi wa kufunga maduka kutokana na vilio vyao kutosikikizwa, hususan oparesheni zinazofanywa mara kwa mara na TRA sokoni hapo, ambazo zimesababisha wateja wao hasa wa kutoka nje ya nchi, kuwakimbia.

Pia, Mbilinyi amesema sababu nyingine ya mgomo huo ni kodi mpya ya maghala ya kuhifadhia mizigo.

Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Honest Kalist, alisema “hapa hakuna kurudi nyuma, hili suala ili liishe salama na wafanyabiashara kufikia malengo Yao inabidi wakutane na Rais, sababu wasaidizi wake wamefika bila mafanikio.”

Mfanyabiashara Bernard Kalumba, alisema wanataka kuzungumza na Rais Samia kwa kuwa wasaidizi wake walishazungumza nao bila mafanikio.

“Makubaliano yetu katika group ni kwamba tunataka kusikilizwa na Rais Samia, kwa Nini tunataka kusikilizwa nae, kwa sababu hawa wasaidizi wake tulishaongea naye akiwemo Waziri wa fedha akasema hakuna mizigo itakayokamatwa lakini hakuna mafanikio yoyote mizigo inaendelea kukamatwa,” amesema Kalumba.

Amos Makala, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam

Baadhi ya wafanyabiashara hao wameweka ahadi ya kuwazuia wenzao watakaojaribu kufungua maduka yao.

Kufuatia maoni hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana aliwataka wafanyabiashara wafanye wanachokitaka, baada ya jitihada zake za kuwatuliza kugonga mwamba.

Hadi MwanaHALISI Online inaondoka eneo la tukio, asilimia kubwa ya wafanyabiashara walikuwa wamefunga maduka yao, huku wafanyabiashara wadogo (wamachijga) wakiendelea kufungua meza zao.

Mtandao huu ulipozungumza na baadhi ya wamachinga sababu zao wao kuendelea na biashara, walijibu “hao wanaogoma ni wakubwa, watajijua wenyewe. Sisi tuna familia watoto Wetu hawali mpaka tuingie barabara, wenzetu wanaogoma wanahela.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the loveBENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani...

Habari Mchanganyiko

NEMC yatoa elimu matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

error: Content is protected !!