Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema waigomea Tume ya marekebisho ya Sheria, wataja sababu saba
Habari za SiasaTangulizi

Chadema waigomea Tume ya marekebisho ya Sheria, wataja sababu saba

Spread the love

CHAMA cha Demokrasis na Maendelea (Chadema) kimewaagiza viongozi wake ngazi kanda, mikoa na majimbo kutoshiriki vikao vinavyotarajiwa kuanza kesho na kuratibwa na Tume ya Marekebisho ya Sheria kwa lengo la kufanya mapitio ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chadema imeitaka Tume hiyo ya marekebisho ya sheria kusitisha kufanya mapitio hayo kwa sababu vikao hivyo vina njama za kuchelewesha mchakato wa kupata Katiba mpya na tume huru ya uchuguzi – mabadiliko ambayo kimsingi yatawezesha nchi kuwa na uchaguzi huru na haki.

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 10 Novemba, 2022 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi yauwepo wa taarifa za tume hiyo kuanza vikao hivyo mfululizo kupitia kwa wakuu wa mikoa.

“Ni njama ambazo kwa bahati ambaya zinafanywa na chombo cha serikali ambacho kipo chini ya wizara ya katiba na sheria hivyo natoa wito kwa mamlaka za serikali, ofisi ya rais na waziri mkuu kusitisha mchakato huo,” amesema.

Amesema Chadema wamefikia uamuzi huo kwa kzuingatia kwamba kwa uzoefu, maoni ya wananchi na uhalisi wa mambo unaonesha matatizo ya kiuchaguzi msingi wake ni mapungufu yaliyopo kwenye katiba ya sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inazalisha mapungufu mengine kwenye sheria mbalimbali.

“Kwa hiyo huwezi kuanza mchakato wa kurekebisha sheria za uchaguzi, bila kufanya mabadiliko kuondoa mapungufu yaliyopo kwenye katiba,” amesema.

Amesema baadhi ya mapungufu ambayo yapo kwenye katiba kabla ya kushughulika na sheria kwenye masuala ya kiuchaguzi ni tume yenyewe ya uchaguzi kwa sababu katiba ya sasa haijaunda tume huru ya uchaguzi kwenye muundo wake, uteuzi, utendaji kazi wake.

“Pili; ukiondoa tume ngazi ya taifa, mfumo mzima wa watumishi wa tume, wakurugenzi wa tume, wasimamizi wa uchaguzi kwenye majimbo, kata na watumishi wengine wa tume, kikatiba wanapaswa kuwekewa mfumo ambao tume huru ndio utawezesha upatikanaji mfumo mzuri wa watumishi wa tume. Jambo hili haliwezi kufanyiwa kazi na sheria peke yake.

“Tatu; matokeo ya urais Tanzania yamezuiliwa kwa katiba kupingwa mahakamani hivyo huwezi kutunga sheria ambayo inaruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani bila kwanza kufanya mabadiliko kwenye katiba.

“Nne; katiba imekataza mgombea binafsi hivyo huwezi kufanya marekebisho ya sheria kuruhusu wagombea binafsi bila kufanya mabadiliko ya katiba.

“Tano; Katiba haijaweka utaratibu ambapo chaguzi za chini iwe za serikali za mitaa na chaguzi nyingine kusimamiwa moja kwa moja na tume huru ya uchaguzi hivyo huwezi kushughulika na jambo hili bila kuanza na katiba.

“Sita; katiba haijaweka utaratibu ambao hata kura ya maoni ya katiba mpya kusimamiwa na tume huru ya uchaguzi.

“Saba;Katiba haijaweka utaratibu ambao katika hatua mbalimbali maamuzi ya tume yanaweza kupingwa mahakamani na mwisho Katiba haijaweka utaratibu ambapo mgombea akiwa mmoja kwenye ubunge anaweza kupigiwa kura ya ndio na hapana lakini kwenye urais imeruhusiwa,” amesema.

Amesema ili kutibu tatizo la kukosekana kwa uchaguzi huru na haki lazima kuanza na katiba mpya kwani kinachofanywa na tume ya kurekebisha sheria, kimsingi ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Amesema Chadema walishalalamikia matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi kwenye kikosi kazi kilichofanya kwa miezi 10 na kukusanya maoni ambayo tayari yalishakusanywa tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Serikali kabla ya kutujibu imetumia kiasi gani kwenye kikosi kazi kilichotuletea mapendekezo yasiyokuwa na muafaka, inaanzisha mchakato mwingine kutumia tume ya kurekebisha sheria kufanya mapitio ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa,” amesema.

Aisha, amesema matatizo yanayohusiana na uendeshaji wa vyama vya siasa ni mianya kutunga sheria ambazo zimetoa mamlaka makubwa ambayo yanatumiwa vibaya na msajili wa vyama vya siasa.

“Ndio maana Rasimu ya Warioba inayotokana na maoni ya wananchi kwamba ofisi ya msajili haipo huru inatumika vibaya, pamoja na kuwa tungeiboresha zaidi ilikuwa na ibara mahususi sehemu ya tatu ilikuwa inahusu masuala ya vyama vya siasa na msajili wa vyama vya siasa ambayo kwenye katiba ya sasa hayapo,” amesema.

Amesema kinachotaka kufanywa na tume ya marekebisho ya sheria kina njia mbaya ya kupenyeza mambo mawili, kwanza kumpa mamlaka makubwa zaidi msajili wa vyama vya siasa kuingilia vyama.

“Pili wana nia ovu kwa kile wanachokiita kuweka utaratibu wa vyama kudhibitiana kwa kuja na mapendekezo yenye nia ovu kimsingi kutumia wingi wa baadhi ya vyama kutawala kudhibiti vyama vya upinzani vyenye msimamo wa kusimamia masuala ya msingi ya demokrasia, uhuru, haki za wananchi na mambo mengine ya mabadiliko ya nchi yetu,” amesema.

Amesema badala yake kama Tume hiyo ya marekebisho ya sheria inataka kufanya kazi yake kitaalamu ijitokeze iwaeleze wananchi ni kwanini mpaka sasa ipo kimya na haijawahi kujiunga kwenye sauti ya kuitaka serikali iondoe zuio la mikutano ya hadhara ya siasa ambalo liko kinyume cha katiba ya nchi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya jeshi la polisi.

Aidha, amesema Chadema inakemea utaratibu huu uliotumiwa na tume ambayo ni kinyume kwa kuruka ngazi za kitaifa za vyama na kurukia kwenda kufanya kikao na viongozi wa chini katika mambo ambayo walipaswa kuwasiliana na ngazi ya kitaifa.

“Tunaona kwamba hiki kinachofanyika kwa sababu hatuna barua yoyote kutoka tume ya marekebisho ya sheria ikituomba maoni au kutualika au kukutana na sisi.

“Wameruka kinyemela wakiwatumia wakuu wa mikoa na wilaya, wale waliitumika kuhujumu uchaguzi 2020, tume ya kurekebisha sheria inawatumia kukusanya maoni ya vyama ngazi ya chini kuhusu mabadiliko yanayohusiana na vyama vya siasa.

“Wito huu umeshuka ghafla na wametuambia na kututumia nakala ya barua ya wito, hivyo tumeona tulisema jambo hili hadharani kwamba viongozi wetu hawatashiriki hivi vikao,” amesema.

1 Comment

  • Mimi nafikiri Chadema, warekebishe jina lao. Kuliko kuitwa : Chama cha democracia na maendeleo, waitwe : Chama cha fujo na kupinga maendeleo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!