WAKATI taarifa rasmi za idadi ya watu waliokuwemo ndani ya ndege ya Precision Air iliyopata ajali leo Jumapili katika Ziwa Victoria mkoani Kagera ikitajwa kuwa ni 43, imebainika kuwa jumla ya watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo ni 45 wakiwamo marubani na wahudumu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bukoba … (endelea).
Hatua hiyo imekuja wakati taarifa ya Jeshi la Polisi pamoja na Kampuni hiyo ya Precision Air zikibainisha kuwa abiria walikuwa 39 akiwamo mtoto mmoja na wafanyakazi wanne.
Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa jioni tarehe 6 Novemba, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila imebainisha kuwa ndege hiyo ilikuwa na idadi ya watu 45.
Amesema wakati wa uokozi imebainika kulikuwa na jumla ya abiria 41 na wahudumu wanne.
“Jumla ya watu 19 wamefariki dunia wakiwemo rubani na msaidizi wake. Aidha waliookolewa ni watu 26 kati yao mmoja baada ya kuokolewa alikimbia na hajulikani alikokwenda,” imesema taarifa hiyo.
Ndege hiyi iliyokuwa inatokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza kupitia Bukoba, ilishindwa kutua katika Uwanja wa Bukoba na kulazimika kutua ziwani.
Aidha, taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha ajali ya ndege hiyo yenye usajili namba 5H-PWF, ni hali mbaya ya hewa hasa upepo ndio uliosababisha rubani ashindwe kutua katika uwanja wa kutua mita takribani 100 ndani ya maji kutoka ziwani.
Chalamila amesema zoezi ka uokoaji limeendeshwa kwa ushirikiano na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na jioni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishitiki zoezi hiko pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
Leave a comment