Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya kupinga Rais, Spika, Jaji Mkuu kutoshtakiwa yatupwa
Habari za Siasa

Kesi ya kupinga Rais, Spika, Jaji Mkuu kutoshtakiwa yatupwa

Spread the love

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeitupilia mbali kesi ya kupinga marekebisho ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (BRADEA) ya 2020, yanayozuia Rais, Spika na Jaji Mkuu, kushtakiwa moja kwa moja mahakamani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Pia, kesi hiyo ilikuwa inapinga yanayozuia mtu kufungua kesi asiyokuwa na maslahi nayo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumanne, tarehe 15 Februari 2022 na Mahakama hiyo mbele ya Jopo la Majaji Watatu wa Mahakama Kuu, Elinaza Luvanda, Yose Mlyambina na Stephen Magoiga.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo madai Na. 09/2021, iliyofunguliwa na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, Jaji Mlyambina alisema marekebisho hayo hayajakiuka Katiba.

 

Jaji Mlyambina alisema, vifungu vilivyofanyiwa marekebisho katika sheria hiyo, havikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa.

Katika hukumu ya kesi hiyo, kuhusu kipengele Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kushtakiwa kwa niaba ya Rais, Spika wa Bunge na Jaji Mkuu, mahakama hiyo ilisema takwa hilo la AG kushtakiwa kwa niaba ya wakuu wa vyombo vingine vya dola liko kikatiba.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa THRDC, Paul Kisabo alidai hawajaridhishwa na uamuzi huo na kwamba wataka rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, wakati wowote kuanzia jana Jumanne.

“Mahakama imetoa uamuzi huo, lakini sisi kama mawakili hatujaridhishwa na maamuzi hayo. Tutakata rufaa Mahakama ya Rufani muda wowote kuanzia sasa,” alidai Wakili Kisabo.

Wakili Kisabo alidai, pamoja na mambo mengine, katika kesi hiyo walikuwa wanapinga marekebisho ya sheria hiyo, yaliyoweka sharti la Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kushtakiwa kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Rais na Spika wa Bunge.

“Lakini pia kupitia marekebisho hayo, sheria hiyo ilitoa hitaji ya kwamba ukihitaji kumshtaki Jaji Mkuu, Rais na Spika, unapaswa kumshtaki tu AG kwa niaba yao. Sisi tuliona hitaji kama hilo sio sahihi, tukafungua kesi hii kwa ajili ya kuinga marekebisho hayo,” alidai Wakili Kisabo.

Katika kesi hiyo ya madai, Olengurumwa alikuwa akipinga kifungu cha 4 (2,3,4 na 5) , cha sheria hiyo, kinachoelekeza mtu anayetaka kufungua kesi mahakamani, lazima athibitishe kuathirika moja kwa moja na suala lililosababisha kufungua kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Olengurumwa, alidai kifungu hicho kinazuia wajibu wa mtu na au taasisi, katika kudhibiti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na kuilinda katiba na sheria za nchi.

Olengurumwa alidai, kifungu hicho kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, misingi ya mgawanyo wa madaraka, utawala wa sheria na utawala bora, kama inavyoelekezwa na matakwa ya katiba hiyo.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu anadai, kifungu hicho kinakiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania iliingia, ikiwemo mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Makataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.

Hoja nyingine ya Olengurumwa, anadai kifungu hicho kimempa mamlaka makubwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kinyume na katiba.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!