July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwili wa Dk. Mwele kuwasili Ijumaa, kuagwa Dar, kuzikwa Dodoma J3

Spread the love

MWILI wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), anayeshughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs), Dk. Mwele Malecela (58), utawasili nchini Tanzania usiku wa Ijumaa, tarehe 18 Februari 2022, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Anaripoti Rhoda Kanuti, Dar es Salaam…(endelea).

Utawasili kwa Ndege ya Shirika la KLM ukitokea Geneva nchini Uswisi ambako Dk. Mwele alifikwa n amauti tarehe 10 Februari 2022 ambapo mazishi yake yatafanyika Mvumi, mkoani Dodoma 21 Februari 2022.

Leo Jumatano, tarehe 16 Februari 2022, Samwel Malecela ambaye ni msemaji wa familia ya waziri mkuu mstaafu, John Malecela, akizungumza na wanahabari nyumbani kwao maeneo ya Sea View, jijini Dar es Salaam amewaomba wananchi kuendelea kumwombea.

“Baada ya kumpokea usiku wa Ijumaa, tutakuja naye hapa nyumbani, ambapo waombolezaji na familia watakuwepo hapa nyumbani, kwa ajili ya kuendelea na maombolezo,” amesems Samweli ambaye ni mdogo kwa Dk. Mwele

“Siku ya Jumamosi asubuhi tutafanya sala fupi hapa nyumbani, ambapo familia watapata nafasi ya kumuaga ndugu yetu,” amesema Samweli.

Msemaji huyo wa familia amesema siku ya Jumamosi kuanzia saa 3.00 asubuhi, misa ya kumsindikiza Dk. Mwele, itafanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Alban.

Kisha majira ya saa 5.00 asubuhi, mwili wake utafikishwa kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutolewa heshima za mwisho kwa watu mbalimbali.

“Tunategemea kwenda Viwanja vya Karimjee mida ya saa 5.00 asubuhi, mbapo tutakuwa na matukio mawili, la kwanza kumpa heshima zake za mwisho kwa maana ya kumuaga,” amesema

Aidha amesema, tutapata salamu mbalimbali kutoka kwenye makampuni, Serikali na watu binafsi watakaoweza kuja kutoa salamu zao za rambirambi.

Samweli amesema, baada ya zoezi hilo kukamilika kwenye Viwanja vya Karimjee, mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kwa ajili ya safari kuelekea jijini Dodoma.

“Dodoma tunategemea kuwepo pale kuanzia saa 12.00 hadi saa 1.00 jioni, baada ya kupokelewa Uwanja wa Ndege wa Dodoma, tutaelekea moja kwa moja Hospitali ya Benjamini Mkapa, ambako tutampumzisha kwa siku hiyo ya Jumamosi,” amesema Samuel.

Mdogo wa huyo wa marehemu Dk. Mwele, amesema siku ya Jumapili mwili huo utafikishwa nyumbani kwao maeneo ya Kilimani majira ya saa 4.00 asubuhi, ambapo wananchi wataitumia siku hiyo kutoa heshima zao za mwisho.

Amesema, kesho yake Jumatatu ya tarehe 21 Februari 2022, itafanyika misa takatifu kwenye Kanisa la Anglican Dodoma Cathedral, kisha mwili utapelekwa Kata ya Mvumi, kwenda kutolewa heshima za mwisho kwa watu wa wilaya ya Chamwino.

Baada ya mwili huo kuagwa Mvumi, utapumzishwa katika makazi yake ya milele.

Dk. Mwele aliyekuwa mtoto wa Malecela, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR), ambapo uteuzi wake ulitenguliwa Desemba 2016 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Hadi umauti unamfika, alikuwa anasimamia miradi ya kupunguza magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele ya WHO, jukumu alilolishika kuanzia Oktoba 2018. Alijiunga na shirika hilo la afya duniani mwishoni mwa 2016.

error: Content is protected !!