Thursday , 9 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge waibana Serikali kodi laini za simu, miamala
Habari za Siasa

Wabunge waibana Serikali kodi laini za simu, miamala

Spread the love

 

BAADHI ya wabunge kutoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, wameishauri Serikali ifungue akaunti maalumu ya benki, kwa ajili ya kuhifadhi fedha zitokanazo na vyanzo vipya vya mapato, vilivyowekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa katika nyakati tofauti, bungeni jijini Dodoma, katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Baadhi ya vyanzo vipya vilivyowekwa, kwa ajili ya kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, ni kodi ya laini ya simu na miamala ya kutuma au kutoa pesa.

Vyanzo hivyo vilitajwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, tarehe 10 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma, akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali pendekezwa, kwa mwaka huo wa fedha.

Akizungumza katika mjadala huo, leo Ijumaa tarehe 18 Juni 2021, Mbunge Viti Maalumu asiye na chama bungeni, Jesca Kishoa, amesema vyanzo hivyo vipya vya mapato viwekewe uzio, ili visitumike kinyume na malengo yake.

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

“Nilikuwa na ombi, ni vyema vyanzo vyote ambavyo vimewekwa kwenye bajeti, vimetengwa kuwa mahususi kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo, viwekewe zuio,” amesema Kishoa.

Mbunge huyo ameshauri fedha hizo ziwekwe katika akaunti maalumu, badala ya kupelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Hazina wa Serikali, hali inayoweza sababisha zipangiwe matumizi mengine.

“Kuwepo akaunti itakayokuwa maalumu kwa ajili ya kutunza vyanzo hivi, mfano tozo ya laini ya simu na miamala ya fedha. Zipewe akaunti maalumu sababu tusipofanya hivyo, tutajikuta tunaingia mtego mbaya,” amesema Kishoa.

Mwanasiasa huyo ameongeza “mtego wa kukusanya tozo hizi tunapeleka katika mfuko wa Serikali, zikapangwe kwenye matumizi mengine. Hili waziri uwe makini, mwisho wa siku utakuja kubeba mzigo ambao utashindwa kuutua.”

Jesca Kishoa

Mbali na uanzishwa akaunti maalumu, Kishoa ameshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, apewe mamlaka ya kukagua fedha hizo, ikiwemo ukusanyaji na matumizi yake, ili kuziba mianya ya ubadhirifu.

“Akaunti hizi CAG apewe mamlaka kamili ya kukagua, kupitia na kuhakikisha fedha zinazokusudiwa katika miradi ya maendeleo, zinaenda kuliko kusudiwa. Hii itawapa imani wananchi kuona fedha wanazochangia, zinaenda moja kwa moja kwenye miradi iliyokusudiwa,” amesema Kishoa.

Naye Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, akizungumza bungeni jana tarehe 17 Juni 2021, aliitaka Serikali ilinde fedha zitakazokusanywa, katika vyanzo hivyo vipya vya mapato.

“Naungana na Serikali kuanzisha kodi hii, isipokuwa matumizi ya pesa hizi yalindwe, yasiende kutumika kwenye maeneo yasiyopaswa kutumika,” amesema Zungu.

Zungu alisema , fedha hizo zikitumika vizuri, zitasaidia kutatua matatizo ya wananchi, kama ukosefu wa huduma za afya, miundombinu mibovu ya barabara na ukosefu wa maji safi na salama.

Mussa Zungu, Mbunge wa Ilala

Akiwasilisha bajeti hiyo pendekezwa , Dk. Mwigulu alisema Serikali imepanga kutoza kodi ya laini ya simu kiasi cha Sh. 10 hadi 200, kulingana na matumizi ya mtumiaji.

Alisema chanzo hicho kipya cha mapato, kitaiwezesha Serikali kupata Sh. 396.3 bilioni.

Pia, alisema Serikali imepanga kutoza Sh. 10 hadi 10,000, katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa, kiwango ambacho kitatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha husika.

Waziri huyo wa fedha alisema, pendekezo hilo litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh. 1.2 trilioni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!