Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mwili wa Magufuli kulazwa Ikulu Zanzibar
Habari Mchanganyiko

Mwili wa Magufuli kulazwa Ikulu Zanzibar

Spread the love

 

MWILI wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli (61) utalazwa katika Ikulu ya Zanzibar, kisha kesho tarehe 24 Machi 2021, utasafirishwa kwa ndege maalumu kuelekea jijini Mwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ratiba  hiyo imetolewa leo Jumanne tarehe 23 Machi 2021 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,  katika shughuli ya kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli, kwenye Uwanja wa Amani, visiwani Zanzibar.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi, amesema mwili huo utalazwa Ikulu ya Zanzibar, ili kuenzi mchango wa Hayati Rais Magufuli katika visiwa hivyo, enzi za uongozi wake.

“Kiongozi wetu aliyelala hapa mbele yetu alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo mwili wake utalala Ikulu ya Zanzibar, na kesho asubuhi mwili utaondoka kwa ndege maalumu kwenda jijini Mwanza,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema baada ya mwili wa Hayati Rais Magufuli  kuwasili jijini Mwanza, utapelekwa nyumbani kwa mjane wake, Mama Janeth Magufuli, maeneo ya Busisi, kupitia katika daraja la Kigongo-Busisi, ambalo alilibuni na kusimamia ujenzi wake, akiwa hai.

Waziri Majaliwa amesema jeneza lenye mwili wa Hayati Rais Magufuli litasimamishwa Busisi kwa dakika 10, kwa ajili ya kutolewa heshima za mwisho.

“Tunatarajia mwili huu utembee kwa gari kutoka Mwanza Mjini kupitia daraja kubwa linalojengwa lililobuniwa na yeye mwenyewe.

Baadaye nyumbani kwa mama wa mke wa marehemu mjini Busisi. Utasimama kwa dakika kumi ili wazee maarufu wa Mji wa Buisisi, ndugu wa mke wa marehemu ambao wako pale wataushuhudia ukipita,” amesema Waziri Majaliwa.

Baada ya mwili huo kutolewa heshima za mwisho mjini Busisi, utapelekwa wilayani Sengerema, Geita Mjini hadi Katoro wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

“Tutafanya hivyo safari kuelekea Sengerema mpaka Geita Mjini na kufika katoro na kuingia kwenye jimbo ambalo rais ameongoza kwa miaka 20, la  Chato.  Na hatimaye kufika mjini Chato,” amesema Waziri Majaliwa.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli leo umeagwa visiwani Zanzibar, baada ya kuagwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Shughuli ya mazishi ya kitaifa ilifanyika jana tarehe 22 Machi 2021, katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, wakiwemo marais tisa wa nchi za Bara la Afrika.

Baada ya Zanzibar, mwili wa Hayati Rais Magufuli kesho tarehe 24 Machi 2021, utaagwa na wananchi wa Mkoa wa Mwanza, kisha tarehe 25 Machi mwaka huu, wananchi wa mkoa wa Geita watatoa heshima zao za mwisho wilayani Chato, mkoani humo.

Zoezi la kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli,  linafanyika kwa siku sita mfululizo, kuanzia Jumamosi ya tarehe 20 hadi 25 Machi 2021, ambapo Ijumaa ya tarehe 26 Machi mwaka huu, utapumzishwa katika makao yake ya milele kijijini kwao Chato mkoani Geita.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

error: Content is protected !!