May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwili Magufuli wawasili Z’bar, Uwanja wa Aman wafurika

Spread the love

 

WANANCHI wa Zanzibar, wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), aina ya Air Bus, iliyobeba jeneza lenye mwili wa Dk. Magufuli, iliruka Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa 2:40 asubuhi na kutua Uwanja wa Abeid Aman Karume saa 3:20 asubuhi. Ikiwa imetumia dakika 40.

Viongozi mbalimbali wamejitokeza kuupokea uwanjani hapo wakiongozwa na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Makamu wa Kwanza wa Rais, Othuman Masoud Othuman, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, mawaziri, watendaji mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi.

Uwanja wa Aman, maelfu ya wananchi wamejitokeza tangu asubuhi ya leo Jumanne tarehe 23 Machi 2021, huku wengine, wakijipanga barabarani kushuhudia msafara uliobebwa ukipita.

Hadi kufikia saa 3 asubuhi, mageti yalikuwa yamefungwa kutokana na idadi kubwa ya waombolezaji waliokuwa wamejitokeza.

Kesho asubuhi Jumatano, mwili wa Dk. Magufuli, utasafirishwa kutoka Zanzibar kwenda Mwanza ambapo utaangwa na wananchi wa mkoani humo na maeneo jirani, katika Uwanja wa CCM Kirumba na baadaye, kusafirishwa kwenda Chato, mkoani Geita.

Utasafirishwa kwa barabara ukipita Misungwi- Sengerema- Geita- Buseresere- Katoro- Bwanga hadi Chato. Maeneo yote hayo inatarajiwa kushuhudia, mamia ya wananchi wakiwa wamejipanga barabarani kumuaga.

Jana Jumatatu, mwili wa Dk. Magufuli uliagwa kitaifa mkoani Dodoma ambapo marais tsa, makamu wa Rais wawili kutoka Bara la Afrika walishiriki shughuli iliyoongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Marais waliohudhuria ni; Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (EAC), Filipe Nyusi wa Msumbiji, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Felix Tshisekedi wa Congo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Wengine ni; Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro), Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Edgar Lungu (Zambia), Mokgweetsi Masisi (Botswana) na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Pia, kulikuwa na waliowawakilisha wakuu wa nchi, wakiwemo, Makamu wa Rais Burundi, Prosper Bazombana, Makamu wa Rais Namibia, Dk. Nangolo Mbumba, Waziri Mkuu Rwanda, Edourdo Ngirente, Waziri wa Mambo ya Nje Angola, Tete Antonio, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Richard Kabonero.

Mwili wa Dk. Magufuli, utazikwa nyumbani kwake, Chato mkoani Geita, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, akiwa ameacha mjane, Janeth pamoja na watoto saba ambao ni; Suzana, Edna, Mbalu, Joseph, Jesca, Yuden na Jeremia.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!