MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe amehoji mamlaka zinazoendesha uchaguzi mkuu kama walimwelewa vizuri Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyeahidi uchaguzi utakuwa huru na haki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Magufuli ambaye ni mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mara kadhaa alisema, Serikali anayoiongoza itahakikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 unakuwa huru na haki.
Leo Jumatatu tarehe 31 Agosti 2020, akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu mwenendo wa uteuzi wa wagombea udiwani na ubunge, Rungwe ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwarejesha ili kuufanya uchaguzi kuwa huru na haki.
Rungwe ambaye pia ni mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, amesema, wagombea wake ubunge na udiwani katika maeneo kadhaa wameondolewa na wengine kushinikizwa kujiondoa ili kuwafanya wagombea wengine kupita bila kupingwa.
“Hawa watu wanafanya vibaya sana. Rais Magufuli amewahi kuahidi uchaguzi utakuwa huru na haki, sasa kwa hali hii unakuwaje huru sasa, hawa wanaofanya hivi kuwaengua wagombea wetu walimsikiliza kweli Rais,” amehoji Rungwe.
Amesema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ina nafasi ya kurekebisha makosa yaliyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi wa udiwani na ubunge kwa kuwarejesha walioondolewa kwa hila.
“Jamani jamani jamani, tuache siasa za nyuma. Tunapitwa na wakati. Kwa nini tunarudi nyuma. Acheni mchezo huo, unamtangaza aliyepita bila kupigwa, hivi kwa nini CCM wanapita bila kupigwa wao tu, sijawahi kuona mpinzani anapita bila kupigwa.”
“Wananchi wana haki ya kusimama na kumchagua wanayemtaka, wakurugenzi lazima watende haki. Nchi si ya mtu mmoja. Watende haki, watu wanaamua huku wewe unabadilisha. Sisi tumechoka kufanyiwa mauvo,” amesema Rungwe.
eliasshiguta@gmail.com