Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Safari: Chadema wamevunja Katiba yao
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Safari: Chadema wamevunja Katiba yao

Spread the love

ALIYEKUWA makamu mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Prof. Abdallah Safari, amekosoa uaamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kuwavua uanachama wabunge wake wanne. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam, Prof. Safari amesema, “Katiba ya Chadema na hata Nchi imevunjwa,” katika kushughulikia wabunge hao.

“Katiba ya Chadema na Nchi, imepiga marufuku mtu yeyote kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya kujitetea, na kwamba utaratibu wa watuhumiwa kujitetea, ulikuwa ukitumika nyakati za nyuma ndani ya chama hicho,” ameeleza.

Chadema kilitangaza wiki iliyopita kuwavua uwanachama wabunge wake wanne. Miongoni mwa wabunge hao, ni Willifred Lwakatare, mbunge wa Bukoba Mjini; Anthony Komu, mbunge wa Moshi Mjini, Joseph Selasini, mbunge wa Rombo na David Silinde, mbunge wa Momba, mkoani Songwe.

Katika maamuzi yake ya kuwafukuza wabunge hao, Chadema kilisema, kimechukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa wabunge wote hao, wamekuwa wakikisaliti chama hicho.

Kamati kuu iliyofikia maamuzi ya kuwafukuza Lwakatare, Komu, Selasini na Silinde, ilikutana jijini Dar es Salaam, tarehe 8 na 9 Mei mwaka huu. Maamuzi ya Kamati Kuu yalisomwa kwa waandishi wa habari na John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema.

Prof. Safari amesema, “hawa jamaa (wabunge) hawakupewa haki ya kujitetea, ni kweli kwa kuwa sheria inasema hivyo, kwamba mtu ambaye hakupewa haki ya kujitetea, uamuzi huo ni batili.”

Amehoji:“Sasa hawa wamepewa fursa ya kujitetea? Hata mtu ambaye hakwenda shule na sio profesa wa sheria, atasema kwa kweli hapa hapana,” amesema.

Amesema, msingi wa kujitetea unatokana na msingi wa haki ya kujitetea unaotokana na kanuni za haki za binadamu mbili.

Akitaja kanuni ya kwanza Prof. Safari amesema, ni ile inayomtaka mtu asiamue shauri ambalo una maslahi nalo, ya pili; kwamba mtu asihukumiwe bila ya kusikilizwa.

“Tulikuwa na kesi ya John Shibuda (alikuwa Mbunge wa Maswa), alitoa kauli tata sana bungeni, tena mbaya sana kushutumu sera za chama, alifika mbali sana lakini alipewa fursa ya kujitetea na Shibuda akapewa karipio.

“Hata Cecil Mwambe (aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Ndanda) mwenyewe, alikuja katika Kamati ya Maadili, tukamsikiliza. Tukaona hana hatia yoyote. Msabaha (Mariam Msabaha) aliitwa mbele ya Kamati Maadili, akapewa fursa ya kujitetea; akajitetea na akaonekana ana hatia, akapewa adhabu ya faini,” amefafanua.

Ametoa mfano pia wa mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na mwenzake Komu, ambao waliitwa mbele ya Kamati Kuu ili kujieleza.

Amesema, “Kubenea na mwenzake Komu, hawakuja kwenye Kamati ya Maadili, wao waliitwa moja kwa moja kwenye Kamati Kuu, lakini walipewa fursa ya kujitetea.

“Sasa sijui hawa kimetokea kitu gani kwamba hawa, hawakupewa fursa ya kujitetea, halafu basi wangepewa onyo, lakini wamefukuzwa. Kitaratibu sio sawa.”

Gwiji huyo wa sheria nchini amesisitiza kuwa “Katiba ya Chadema hairuhusu mtu ama mwanachama yeyote kuhukumiwa pasi na kusikilizwa.”

Mariam Msabaha, Mbunge Viti Maalum Zanzibar kwa tiketi ya Chadema

Hata hivyo, ameonesha wasiwasi wa uamuzi wa kusamehe na kuwapa nafasi ya kujitetea wengine ambao walifanya kosa la aina moja, la kutotii maagizo ya chama.

“Kwa sababu hata Katiba ya Chadema yenyewe hairuhusu vitu kama hivyo. Na kuhusu wale wengine (waliopewa nafasi ya kujieleza), hapo ndio inashangaza zaidi, kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano inakataza ubaguzi wa aina yoyote hasa katika utoaji haki.

“Hata ukisema, hawakuwa wakiita press conference (mkutano na wanahabari), walikuwa wamekaa, lakini wamefanya makosa kwa sababu, uamuzi wa pamoja (chama) wameupinga,” amesema Prof. Safari.

Mbali na wabunge hao kutimuliwa, wabunge wengine 11 wametakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua akiwamo Mriam Msabaha (Viti Maalum), ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema aliyevuliwa nyadhifa zake zote na kubaki na ubunge pekee.

Wabunge wengine ni; Susan Maselle, Joyce Sokombi, Rose Kamili, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Lucia Mlowe, Lucy Magereli na Dk Sware Semesi (wote Viti Maalumu).

Wengine, ni Willy Qambalo (Karatu), Peter Lijualikali (Kilombero) na Japhary Michael (Moshi Mjini).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

error: Content is protected !!