Sunday , 5 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Vyama sita vya wakulima vyapewa siku 16 kutema mamilioni
Habari za Siasa

Vyama sita vya wakulima vyapewa siku 16 kutema mamilioni

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, imetoa siku 16 kwa vyama sita vya ushirika kurejesha mamilioni ya wakulima wanayodaiwa kabla ya hatua kali za kisheria kuchukuliwa. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, tarehe 15, 2020, jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa ya uchunguzi wa matumizi ya fedha za vyama vya ushirika.

Amesema mpaka sasa, wamefanikiwa kuokoa Sh.11.3 bilioni kutokana na uchunguzi huo walioufanya baada ya kupewa jukumu hilo na Waziri wa Kilimo, Japhat Hasunga tarehe 26 Novemba, 2020.

Bosi huyo wa Takukuru amesema, Waziri Hasunga alichukua jukumu hilo kutokana na tuhuma mbalimbali kuhusu vitendo vya ubadhirifu na rushwa katika matumizi ya fedha za vyama vya ushirika Tanzania.

Kuhusu vyama hivyo sita, Brigedia Jenerali Bungo amesema, licha ya vyama hivyo kufahamu kuwa vinadaiwa fedha za wakulima na kupewa muda wa kurudisha fedha hizo, bado havijaanza kufanya marejesho yoyote.

“Ninaviagiza vyama hivi, kuanza kurejesha fedha wanazodaiwa na wakulima haraka iwezekanavyo, na kwamba baada ya mwezi huu huu wa Mei kuisha, hatua za kuwakamata wamiliki na viongozi wa vyama hivyo kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa dhidi yao, bila ya kuwa na taarifa nyingine ya tahadhari kwao,” amesema Brigedia Jenerali, Bungo

Hii ina maana kuwa, kuanzia leo tarehe 15 hadi 31 Mei ni siku 16 ambazo  zilizotolewa na Takukuru kwa vyama hivyo kurejesha mamilioni hayo ya fedha.

Amevitaja vyama hivyo na kiwango wanavyodaiwa kwenye mabano ni; Chama cha KYEKU LTD cha jijini Mbeya (Sh.476 milioni), Chama cha TANECU  LTD cha korosho Mtwara (Sh.359 milioni) na Chama cha NEEMA SCCOS LTD cha mkoani Njombe (Sh.234 milioni).

Vingine ni; Chama cha MAMCU cha korosho kilichopo Mtwara (Sh2.5 bilioni), Chama cha RUNALI kilichopo Nachingwea mkoani Lindi (Sh.856 milioni) na chama cha SCCULT cha jijini Dar es Salaam kinachodaiwa Sh 4.8 bilioni.

Brigedia Jenerali, Bungo amesema kupitia operesheni hiyo, wamefungua majalada ya uchunguzi 79 katika mikoa mbalimbali nchini.

“Zipo kesi 11 zinazoendelea katika mahakama zetu nchini. Yapo majadala tisa ambayo yapo katika mchakato wa kukamilisha ili tuweze kufikisha watuhumiwa mahakamani,” amesema

Amesema yapo majalada yaliyokamilika na kufungwa baada ya fedha zinazodaiwa kurejeshwa zote au hoja zilizokuwa zililalamikiwa zimejibiwa zote na pande zote kuridhika.

“Yapo majalada yanayoendelea na uchunguzi kwa kuwa japokuwa fedha zilizokuwa zikidaiwa zimeanza kurejeshwa lakini uchunguzi umebaini tuhuma za wizi na ubadhirifu,” amesema

Amesema yapo majalada ambayo fedha zilizokuwa zinadaiwa zinaendelea kurejeshwa lakini pia kuna kesi zinazoendelea mahakamani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mbatia ambwaga Selasini, mahakama yaamuru alipwe fidia

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemuamuru...

Habari za SiasaTangulizi

Mkulo afariki dunia, kuzikwa kesho Kilosa

Spread the loveALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa...

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

error: Content is protected !!